Thursday, March 12, 2020

Simba yamalizia hasira kwa Singida United

Miamba ya soka Tanzania Simba SC imetoa dozi ya msimu baada ya kuizabua Singida United kwa mabao 8-0 ikiwa ni kichapo kikubwa kutoa tangu kuanza kwa Ligi Kuu 2019/2020.

Ushindi huo umekuja baada ya kupoteza katika mchezo uliopita wa Machi 8 dhidi ya watani zao Yanga.

Mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ulishuhudiwa mshmabuliaji wa Rwanda Meddie Kagere akifunga mabao manne katika dakika ya 2, 26, 41 na 71.

Mabeki wa Singida United, wakiongozwa na Tumba Swedi 'Mdudu Kiwi' ambaye aliwahi kutamba akiwa Stand United, walishindwa kumdhibiti mshambuliaji huyo hatari.

Mabao manne ya Kagere katika mchezo huo, yamemfanya kuendelea kujitengenezea mazingira akiwa na mabao 19 ya kubeba kiatu cha mfungaji bora kwa msimu wa pili mfululizo.

Mabao mengine ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Deo Kanda ambaye alitupia mawili, John Bocco na Sharaf Shiboub waliofunga bao moja kila mmoja.

Ndani ya dakika zote za mchezo Simba walionekana kumiliki mpira kwa asilimia kubwa huku kocha wa kikosi hicho akionekana kufanya mabadiliko kadhaa kwa madhumuni ya kuwapumzisha wachezaji wake baada ya kuwa na uongozi wa mabao mengi, akiwemo Shomary Kapombe.

Katika mchezo huo, Singida United iliwalazimu kumaliza wakiwa pungufu baada ya kiungo wao, Haruna Moshi 'Boban' kuonyesha kadi nyekundu baada ya kuchezea vibaya, Aishi Manula.

Kikosi cha Simba, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Tairone Santos, Pascal Wawa,Jonas Mkude, Deo Kanda, Luis Miquissone, Meddie Kagere, John Bocco na Hassan Dilunga.


Kikosi cha Singida United, Owen Chaima, George Wawa, Haji Mwinyi, Meshack Kibona, Tumba Swedi, Cleophace Sospeter, George Sangija, Haruna Moshi 'Boban', Steven Sey, Seiri Arigumaho na Mtikila Hussein.


0 Comments:

Post a Comment