Saturday, March 14, 2020

Unaikumbuka siku Zaire walipotwaa taji la pili la Afrika 1974?

Machi 14, 1974 timu ya taifa ya soka ya Zaire wakati huo ambayo kwa sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitwaa taji la pili la Mataifa ya Afrika kwa kuizabua Zambia kwa mabao 2-0. 

Zaire ilitwaa taji la kwanza mnamo mwaka 1968 wakati huo ilikuwa ikifahamika kwa jina la Kongo-Kinshasa kwa kuidungua Ghana kwa bao 1-0. 

Hata hivyo mnamo mwaka 1970 ilitolewa katika mashindano hayo katika mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi. Mnamo mwaka 1972 Zaire ilifanikiwa kumaliza nafasi ya nne ya mashindano hayo. 

Katika mashindano ya mwaka 1974 ilifika fainali kutokana na kazi nzuri ya kiungo Ndaye Mulamba alifunga mabao matano katika hatua za mwanzo ikiwamo mechi ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Misri katika nusu fainali. 

Katika mchezo huo wa nusu fainali Mulamba Ndaye alifunga mabao mawili yaliyowapeleka fainali. Mnamo Machi 12 katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo Mulamba Ndaye alifunga bao katika sare ya 2-2 baada ya muda wa ziada iliyowafanya mchezo huo urudiwe dhidi ya majirani Zambia. 

Siku mbili baadaye walikutana katika mchezo mwingine hapo hapo jijini Cairo. Katika mchezo huo wa marudiano Mulamba Ndaye alifunga katika dakika ya 30 na 76 hivyo Zaire kuwa mbele kwa mabao 2-0. 

Hadi michuano hiyo inamalizika Mulamba Ndaye alikuwa amefunga mabao 9 na kuwa mfungaji bora. 

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo haijafanikiwa kurudi tena katika fainali kwani mara ya mwisho iliishia kushika nafasi ya tatu katika michuano hiyo mwaka 1998.
Mulamba Ndaye

0 Comments:

Post a Comment