Monday, March 9, 2020

Simbu kushiriki St. Patrick Half Marathon Arusha


Mwanariadha wa Tanzania Alphonce Felix Simbu anatarajiwa kuwa miongoni mwa wanariadha watakaochuana katika mbio za St. Patrick zitakazofanyika mkoani Arusha Machi 14 mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili Mratibu wa mbio hizo Mwalimu Denis Shemtoi alisema ujio wa Simbu katika mbio hizo ni jambo muhimu katika kusherekea siku ya St. Patrick ambayo huadhimishwa kila mwaka.

"Simbu ni mwanariadha mkubwa na mwenye heshima hapa nchini, alikwenda na kutuwakilisha vizuri katika olimpiki, tumezungumza naye na amethibitisha kuwa atashiriki mbio hizi," alisema Shemtoi.

Shemtoi alisema mbio hizo za kilometa 21 zitaanzia katika Mbuga ya Wanyama ya Arusha(Arusha National Park) wilayani Arumeru na zitamalizikia Mount Meru katika jiji la Arusha.

" Mbio zitaanza saa 1:00 asubuhi katika mbuga za wanyama, na zitatia nanga Mount Meru ambako hafla nzima itafanyika ikiwamo utoaji wa zawadi. Mbio hizi zinaanzia wilaya ya Arumeru ilipo Arusha National Park na kumalizikia wilaya ya Arusha mjini," aliongeza.

Mratibu huyo alisema madhumuni ya mbio hizo ni kutangaza utalii wa ndani pia kuendelea kuutangaza mchezo wa riadha nchini ambao una historia nzuri nchini kwani ndio mchezo wa kwanza kuipa Tanzania medali ya olimpiki.

"Riadha ndio mchezo pekee ambao ulileta medali ya olimpiki, hatuwezi kuuacha hivi hivi lazima tuendelee kuupa sapoti , lakini pia vivutio vya utalii kama mbuga za wanyama hatuwezi kuacha kutangaza kupitia mbia hizi tumeamua iwe hivyo," alisema Shemtoi.

Aidha kila mshiriki aliyepata namba ya mbio hizo atapata medali yake ya ushiriki na washindi watapewa zawadi zao. 

0 Comments:

Post a Comment