Saturday, March 14, 2020

Waziri Lukuvi atoa maagizo nyeti Maafisa Ardhi Wilaya

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, amewataka maafisa ardhi katika wilaya zote hapa nchini kuhakikisha kwamba wanasimamia upangaji  wa matumizi ya ardhi ndani ya wilaya na mikoa ili wananchi wasiendelee kujenga kiholela.

Lukuvi alitoa maagizo hayo Machi 10, 2020 mkoani Kilimanjaro, wakati akizungumza na wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro, Wakurugenzi, pamoja na maofisa wengine wa serikali wakiwemo maofisa ardhi wa wilaya hizo za Mkoa wa Kilimanjaro.

Aliwataka maofisa hao   kuainisha maeneo ya vijijini ambayo maisha ya watu wake yamebadilika ili yatangazwe kuwa sehemu ya mipango miji ili waweze kupimiwa ardhi hiyo na kumilikishwa.

“Yapo maeneo ndani ya vijiji ambayo watu walioko huko maisha wanayoishi ni ya kimji lakini ardhi ni za vijiji, maeneo ya aina hii yaleteni kwangu tuyatangaze kuwa town planning areas, ili wananchi wapangiwe vizuri wamilikishwe hati za kimji ili walipe kodi”, alisema.

Hata  hivyo Waziri Lukuvi,  aliwakumbusha  Wakurugenzi wa halmashuari za wilaya kuwa mamlaka ya upangaji wa ardhi bado ni jukumu la wilaya, hivyo kila wilaya ina jukumu la kupanga kupima na kumilikisha ardhi na kwamba wakurugenzi wa halmashauri za wilaya wamepewa jukumu la kusimamia, kupanga,  kupima na kumilikisha ardhi.

“Wakurugenzi  napenda  kuwakumbusha kuwa jukumu hili ni la kwenu, mmekuwa mkifikiria ni jukumu la Wizara hapana, jukumu hili ni lenu, nani ataishi wapi au atalima wapi ni jukumu lenu, hata wale wanaoishi kwenye maeneo hatarishi, swala hilo lisingekuweko iwapo Wakurugenzi mngekuwa mnatekeleza majukumu yao kama waamuzi wa matumizi sahihi ya ardhi”, alisema Waziri Lukuvi.

Pia aliwataka kuwapa maofisa ardhi ushirikiano na kuwapa maelekezo watendaji wa sekta ya ardhi waliopangiwa kwenye maeneo yao ili kufanikisha utendaji katika sekta ya ardhi katika maeneo yao.

“Maofisa ardhi hawaji kwenu kuja kuwaelekeza bali nyinyi ndiyo mtawapangia majukumu ya kufanya kuhusiana na ardhi katika maeneo yenu kwa mujibu wa sheria, mkishapanga mnatutumia sisi Wizarani ili kuidhinisha, lazima kila ardhi ipangiwe matumizi yake mijini na vijijini”, alisisitiza.

Aliongeza kusema kuwa “Ardhi iliyopangiwa matumizi yake na watu kupewa hati inaongeza thamani ya ardhi na kukuza uchumi wa mwenye ardhi na wilaya husika kwa kuongeza mzunguko wa fedha kwa kuwa watu watakuwa wanakopesheka maana wana hati ambayo ni dhamana inayokubalika na taasisi za fedha”.

Waziri Lukuvi aliendelea kusema kuwa kuzipa ofisi za ardhi za mikoa majukumu yaliyokuwa ya ofisi za Kanda kutaondoa ukiritimba ambao wananci walikuwa wanakumbana nao wakati wa kutafuta hati, ambapo alisema ni marufuku mwananchi kufuata hati mkoani.

“Mwananchi atapata hati yake palepale katika wilaya aliyoilipia tangu alipoanza mchakato wa kupata hati, msajili atawajibika kuweka ratiba kila mwezi na kutoa taarifa kwa wanaongojea hati zao kwenye wilaya husika siku atakapowapelekea hati zao”, alisema.

Aidha alisema mdhamini wa ardhi atakuweko kwenye ofisi ya Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba hakutakuwa na haja ya mtu kwenda Dodoma kwa ajili ya shughuli hiyo ya uthaminishaji ardhi kama ilivyokuwa hapo awali.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EMAIL: eliaskisena@gmail.com
DATE: Machi 10, 2020

0 Comments:

Post a Comment