Saturday, March 14, 2020

Kirigini: Serikali inaendelea kuboresha sekta ya Afya

SERIKALI inaendelea na jitihada zake za kuboresha utoaji wa huduma za afya hususan maeneo ya vijijini kwa kujenga vituo vya afya, zahanati na hospitali lengo likiwa ni kumuondolea adha mwananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia Jumuiya ya Wazazi  Paulo Kirigini, wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa Sektarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro.

“Nimepita hapa kwa ajili ya kuwasalimia, wote mnafahamu jinsi CCM na Serikali tunavyoshirikiana, ninyi ni Watendaji lakini sisi tunaisimamia Ilani hivyo, nimefurahishwa sana na mapokezi makubwa haya niliyoyapata kutoka kwenu, lakini pia Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa sana,  katika Nyanja za afya elimu, maji na barabara,”alisema.

Awali akitoa taarifa ya mkoa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Khatibu Kazungu alisema serikali inaendelea na jitihada zake za kuboresha sekta ya afya ambapo hadi sasa mkoa huo umejenga vituo vya afya nane na hospitali mbili.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. John  Magufuli serikali imefanikiwa kuboresha huduma za afya kutokana serikali hiyo kuwekeza wataalam pamoja na vifaa tiba.

Dkt.  Kazungu alisema  kuwa utoaji wa huduma  katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Mawenzi, uimarishwa kwa kuwepo kwa vifaa tiba pamoja na wataalam katika maeneo mbalimbali.

Alisema kuwa katika uboreshaji  huo wameongeza vitanda hadi kufikia 300 hali ambayo imefanya wagonjwa wote kulazwa kwenye vitanda pamoja na kupunguza vifo vya wajawazito kwa asiliamia 100.

Dkt. Kazungu  alisema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt.Magufuli hospitali hiyo imefanikiwa kufanya upasuaji wa kuondoa ukungu wa jicho kwa wagonjwa 640 pamoja na kupandikiza kioo cha jicho kwa wagonjwa watatu.

“Hospitali imepunguza rufaa mbalimbali kwa wagonjwa ikiwa ni serikali kuwekeza kwa vifaa na mashine za kisasa hii kwetu imetufanya kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine”alisema Dkt. Kazungu.

Aidha Dkt. Kazungu  alisema kuwa serikali katika uwekezaji  wake imejenga jengo la kisasa lililogharimu  Sh milioni 800 kwa ajili ya magonjwa ya mlipuko ambapo liko katika hatua za mwisho ya kuanza kutumika hali ambayo itasaidia kuboresha huduma za afya kwa magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

“Tangu kuingia kwa serikali ya Awamu ya Tano upatikanaji wa dawa katika hospitali hiyo ni asilimia 90 lakini tutafikia asilimia 100 kutokana na mikakati ya serikali ya uwekezaji kwenye sekta ya afya, vilevile  serikali imejenga jengo la mama na mtoto pamoja na huduma zote zitakuwa katika jengo hilo,”alisema.

“Katika mwaka wa fedha 2019/2020 tumeshapokea Shbilioni 6 za ujenzi wa vituo vya afya katika mkoa wetu wa Kilimanjaro, tumeshajenga vituo vinane vya afya na hospitali mbili katika wilaya ya Rombo na Siha,”alisema Dkt Kazungu.

Hata hivyo baada ya kupokea taarifa hiyo Mjumbe huyo alielekea Wilayani Mwanga  katika kituo cha afya Lembeni na  kumetoa msaada wa mashuka 100 yenye thamani ya Sh milioni 2 kwa ajili ya wagonjwa wanaolazwa hapo hasa wodi ya watoto na akina mama.

Akikabidhi msaada huo Kirigini, alisema msaada huo umetolewa kutokana na mahitaji ya kituo hicho cha afya na kuunga mkono jitihada za uongozi wa halmashauri ya wilaya za kuboresha huduma za matibabu.

0 Comments:

Post a Comment