Wednesday, March 4, 2020

Chama Cha Wanawake Wafanyabiashara mkoa wa Kilimanjaro, (TWCC) kimeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuifanyia marekebisho sheria, kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa na halmashauri hapa nchi.

Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Chama Cha Wanawake Wafanyabiashara Mkoa wa Kilimanjaro (TWCC) Joyce Ndossi, wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake katika kuelekea siku ya Wanawake duniani ambapo katika mkoa wa Kilimanjaro maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya Uhuru Park Machi sita mwaka huu.

Bi. Ndossi  alisema suala la utoaji wa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu, limekuwa ni changamoto kubwa hasa utoaji wa asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Alisema fedha hizo zimekuwa na changato kubwa, kwani kuna sheria ilikuja kwa ajili ya kuwa na vikundi vya watu watano watano, hili limekuwa ni changamoto kubwa, huko nyuma kulikuwa na vikundi vingi ambavyo vilikuwa na hamasa lakini kwa sasa hakuna tena hiyo hamasa, wanaona ni ngumu.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwawezesha vijana kiuchumi ili waweze kuanzisha au kuendeleza shughuli za uzalishaji mali, hivyo ilianzisha kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwa lengo la kutoa mikopo yenye riba nafuu, lakini kwa sasa vikundi vimerudi nyuma kutokana na sheria hiyo mpya kutolewa,”alisema.

Aliongeza kusema kuwa “Tunaliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria hii ibadilishwe kwani imekuwa na changamoto kubwa sana, ni vyema  sheria iliyokuwepo hapo awali irudishwe, ili vikundi  viweze kupewa fedha hizo, ili kila kijana mmoja mmoja aweze kupata fursa ya mkopo utakaomsaidia kuazisha au kuendeleza miradi mbalimbali itakayomkwamua kiuchumi,”alisema Bi. Ndossi.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Moshi Bi. Rose Minja, alisema ukatili dhidi ya wanawake na watoto umekuwa ni changamoto kubwa katika mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema Manispaa ya Moshi, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba watu wanaoendelea na ukatili huo wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha Bi. Minja  alifafanua kuwa katika maadhimisho hayo ya siku ya wanawake  duniani, jumla ya vikundi 37 vitapatiwa  mikopo yenye thamani ya Sh milioni 350 ambapo vikundi vya wanawake ni 22, vijana 14 na kikundi cha watu wenye ulemavu kimoja.

Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Kitaifa yatafanyika Mkoani Simiyu tarehe 08 Machi, 2020 na Kauli mbiu ni “Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa na Baadaye” inayosisitiza kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa uwepo wa usawa wa kijinsia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

STORY BY: Kija Elias
DATE: Machi 3, 2020

0 Comments:

Post a Comment