Monday, June 27, 2022

Mawasiliano mabaya ndani ya familia chanzo cha migogoro

 

“Ukatili huu pia unajengeka ndani ya watoto  pindi wanapoona  wazazi wanatofautiana, wanagombana na hivyo watoto nao kuhamisha ukatili huo kwa watoto wengine au kwa familia zao baadae,” anasema Sr. Christina Nakey wa Chuo cha Montessori, Usharika wa Neema.

 

Huwezi kustaajabu unaposikia mke na mume wakipigana mbele ya watoto wao? Umewahi kujiuliza nini chanzo cha hayo yote?

Mkuu wa Chuo cha Montessori Usharika wa Neema mkoani Kilimanjaro Sr. Christina Nakey anaweka bayana kuhusu chanzo cha migogoro hiyo katika familia nyingi nchini na namna ya kupambana na changamoto hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum wakati wa Kongamano la Mawasiliano ya Amani (NVC) lililofanyika jijini Arusha Sr. Christina anasema, “Kongamano hili limekuwa la baraka na manufaa makubwa sana kwetu, na tuna imani kwamba litakwenda kuzaa matunda mengi Kwa ajili ya jamii yetu.”

Sr. Christina anasema changamoto kubwa ya familia zilizo nyingi ni ukosefu wa mafunzo ya kujitambua ambayo ni muhimu kwa ustawi wa jamii yoyote duniani.

“Kongamano hili litasaidia , kwanza mwenyewe kujisikiliza ndani na kujielewa , kujitambua, ili uweze kuwasikiliza wengine katika njia inayopasa ili uweze kuwaelewa na wao wakuelewe,” anasema Sr. Christina.

Mawasiliano mabaya miongoni mwa watu kuanzia ngazi ya familia imekuwa ni sababu kubwa ya migogoro mingi kuibuka katika jamii hali ambayo imetengeneza makundi.

“Migogoro mingi inatokea kwa sababu tunashindwa kujisikiliza wenyewe ndani ya mioyo yetu hata kuwatafsiri wengine kama ambavyo wanajiona wenyewe na kuwatafsiri vingine,” anasema Christina.

Aidha Sr. Christina anasema madhara makubwa yametokea katika jamii kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wa mitaani na maadili yameshuka kwa kiasi kikubwa.

“Familia nyingi zinatengana na hivyo kusababisha na watoto kuendelea kuteseka Kwa ajili ya ukatili unaotendeka ndani ya familia hizo na kuwa na kundi kubwa la watoto mayatima. Baba kutomsikiliza Mama na mama kutomsikiliza baba na watoto kutokulekewa katika misingi iliyo imara kutokana na mafarakano yaliyomo ndani ya familia,” anaongeza Sr. Christina

Hata hivyo Sr. Christina anatoa wito wake kwa jamii kujitahidi kuwa  na uelewa wa namna ya kuwasiliana pasipo kutokea kwa migongano kutokana na kwamba mawasiliano mazuri ndio chanzo kikubwa cha jamii bora.




0 Comments:

Post a Comment