Mkuu wa Wilaya ya Rombo Kanali Hamisi Maigwa akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya Ulinzi Shiriki katika tarafa za Useri na Tarakea katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo Mamtukuna Juni 29, 2022. |
Mkuu wa Wilaya ya Rombo Kanali Hamisi Maigwa amezindua upya mkakati wa ulinzi shiriki wilayani humo ili kuondoa mazingira ya uhalifu katika makazi ya watu ambao unazidi kutishia maisha ya watu na mali zao.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa zoezi hilo kwa vikundi maalum katika tarafa za Useri na Tarakea Kanali
Maigwa alisema hatua hiyo inajiri kutokana na matukio ya uhalifu yanayozidi
kujitokeza wilayani humo.
“Msiseme suala hili (ulinzi
shirikishi) ni la polisi…watu wengi waliofanikiwa hapa duniani, wanaofanya kazi
za kujitolea;…nia ya kweli ndiyo ninayoitaka, nataka tushikamane katika
hili,tuwe kitu kimoja…acheni kusemanasema, mnakaa mnatuhumianatuhumiana
kwanini?” alisema Kanali Maigwa.
Kwa upande wao washiriki
wa kampeni kabambe ya ulinzi shirikishi walisema kumekuwa na kundi kubwa la
vijana wa Kitanzania waliokimbilia nchini Kenya kurudi wilayani humo huku
wakiwa na tabia za wizi na unyang’anyi.
Aidha sungusungu hao
walisema siku za soko kumekuwa na raia wengi wa Kenya wanaobaki au kuchelewa
kurudi kulingana na sheria za mpakani zinavyotaka hali ambayo imekuwa ikileta
usumbufu.
Suala la wanyamapori
kuibuka nyakati za usiku kwa baadhi ya vijiji wilayani humo limekuwa kikwazo
kikubwa kwa ulinzi shiriki.
Hata hivyo sungusungu
wamemwomba mkuu wa wilaya huyo kupata zana zenye kiwango cha juu ili
kukabiliana na wahalifu pindi wanapojitokeza katika maeneo yao.
“Wafugaji wa Kimasai
wamekuwa wakivamia vijiji vya wakulima wakiwa na zana kama upinde, mishale,
mkuki, visu na mapanga hali ambayo imekuwa ikizidisha wasiwasi,” alisema .
Hata hivyo Mrakibu Msaidizi wa
Polisi wilaya ya Rombo OCD Geofrey Gulenga alisema kuna watu wamekuwa
wakishughulisha na uuzaji wa mirungi, unywaji wa pombe uliopitiliza ambao
umekuwa chanzo cha ukatili kwa wanawake na watoto.
“Katika ngazi zetu kuanzia
mtaa, kitongoji; serikali ya kitongoji ikisimamia vizuri kitongoji kitakuwa
salama; kijiji kikisimamia kuhakikisha eneo lao linakuwa salama litakuwa
salama; mifumo hii ya serikali inatakiwa ifanye kazi kwelikweli ikitegemea
jeshi la polisi kwa kila kinachotokea tutagundua kuwa tumekwama…kutokana na
polisi kuwa wachache na vitendea kazi haviko vya kutosha,” alisema OCD Gulenga.
Akijibu baadhi ya
changamoto za uhalifu wilayani humo Mkuu wa Wilaya alisema kuna upungufu wa
Jeshi la Akiba wilayani humo na kwamba wanaendelea kulifanyia kazi suala hilo
ikiwamo kuongeza wanafunzi wa mafunzo hayo.
Kanali Maigwa alisema
uaminifu miongoni mwa sungusungu na jamii kwa ujumla itapunguza uhalifu na
kukuza maendeleo huku akisisitiza umoja miongoni mwao ndiyo suluhisho la
kuondoa uhalifu huo.
Aidha Kanali Maigwa
alihitimisha kwa kusema, “Sisi kama serikali tukizubaa au tukalemaa tusiweke
nguvu ya kutosha kwa walipa kodi halali wa serikali itafika sehemu serikali
hata mapato yake yatashuka kwasababu vibaka na wezi wamelenga kuwaibia
walipakodi hao…suala la ulinzi shiriki ni la kila mtu,” alisema mkuu wa wilaya.
0 Comments:
Post a Comment