Monday, June 6, 2022

Mkimbiza Mwenge 2022 awaonya watendaji, wakurugenzi miradi ya maji

Mkimbiza Mwenge Kitaifa mwaka 2022 Sahil Nyanzabara Geraruma akizungumza wakati wa kuukabidhi mwenge wa uhuru kutoka Tanga kwenda Kilimanjaro kwenye hafla iliyofanyika katika kijiji cha bendera wilayani Same


SAME, KILIMANJARO

Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa mwaka huu Sahil Nyanzabara Geraruma amewataka watendaji na wakurugenzi kuilinda miradi ya maji iliyofunguliwa ili kuendana na mpango wa serikali wa kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumza katika siku ya kwanza ya kuukimbiza mwenge katika mkoa wa Kilimanjaro Geraruma amesema mpango mkuu wa serikali ni kuifanya miradi ya maji kudumu zaidi na ndio sababu ya kuipa fedha ya kutosha kwa ajili ya kuijenga.

Geraruma amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametumia nguvu kubwa kuitafuta fedha kwa ajili ya miradi hiyo hivyo watendaji na wakurugenzi wanapaswa kuitumia kwa umakini mkubwa ikiwamo ujenzi wa miundombinu yenye hadhi na itayodumu muda mrefu.

Katika uzinduzi wa mradi wa maji wa Kisiwani Barazani wilayani Same ambako mwenge wa uhuru ulipokelewa kutoka mkoani Tanga mkimbiza mwenge huyo alizindua mradi huo uligharimu kiasi cha shilingi milioni 535.

Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Kisiwani Barazani Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani Same Mhandisi Alphonce Mlay amesema mradi huo ulianza kutekelezwa na mkandarasi  kwa mkataba wa shilingi 722.

“Makusudi makubwa ya wilaya ya Same ni kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi ambapo mpaka sasa asilimia 76 ya upatikanaji wa majisafi na salama imewafikia wananchi ikilinganishwa na asilimia 61 kwa mwaka 2015,” amesema Mhandisi Mlay.

Mhandisi Mlay ameongeza kuwa kutokana na kusuasua kwa mkandarasi kuanza serikali iliamua kuvunja mkataba huo na kuanza upya hivyo kuokoa kiasi cha shilingi milioni 196.

“Ujenzi wa mradi wa Maji Kisiwani una chanzo cha mserereko na unahusisha ujenzi wa tenki la lita 200,000; ujenzi wa mtandao wa mabomba yenye urefu wa km 21, ujenzi wa vituo 24 vya kuchotea maji, ujenzi wa tenki dogo la kuvunjia kasi klenye mfumo wa kutibu maji , ujenzi wa chanzo cha pamoja na uwekaji wa fensi katika tenki,” amesema Mhandisi huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicgho Isaac Mrutu amesema, “ Ni mradi mzuri ambao Mama Samia ameona ni vizuri kumtua Mama Ndoo Kichwani, kijiji chetu kilikuwa hakina kabisa na sasa kinapata maji kwa urahisi pia mji huu unapanuka sana. Tumefurahi sana kupata mradi huu. Tumeandaa mikakati ya utunzaji wa mradi huu tutaungalia kwa hali na mali.”


 

 

   

 


0 Comments:

Post a Comment