Thursday, August 12, 2021

Chifu Mwariko ataka chanjo ya Uviko-19 iende kwa wanyamapori


Chifu Athumani Omary Mwariko 'Mhelamwana'

Chifu Athumani Omary Mwariko 'Mhelamwana' ameishauri serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuangalia upya namna ambavyo wanaweza kupambana na janga la Covid-19 kwa wanyamapori ili kuzuia maambukizi mapya ya virusi hivyo.

Hayo yanajiri wakati serikali ikiendelea na utoaji wa chanjo ya maradhi hayo katika mikoa mbalimbali nchini huku sintofahmu ikitawala miongoni mwa jamii licha ya hiari kuwepo kwa anayetaka kuchanjwa.

Akizungumza na gazeti LaJiji Chifu Mwariko alisema virusi vilivyo vingi vimekuwa vikisambaa kupitia wanyama kisha kuingia katika mwili wa binadamu na kusababisha madhara makubwa.

“Virusi vimekuwa hatari sana kwa binadamu, kwani vilivyo vingi vimekuwa vikianzia kwa wanyamapori kisha kusambaa kwetu, nafikiri na ninatoa ushauri kwa serikali kuona namna ambavyo wanaweza kutoa chanjo hata kwa wanyamapori,” alisema Chifu Mwariko.

Chifu Mwariko kutoka katika jamii ya Waseuta wa Kizigua alisema utalii ni muhimu katika mbuga zetu kwani umekuwa kitovu cha uchumi wa Tanzania hivyo tahadhari ni vema zikachukuliwa ili kuifanya sekta hiyo kuendelea kutoa matunda yanayokusudiwa.

“Tumekuwa tukiitegemea sekta ya utalii, tuna mbuga za wanyama ambao nao uchunguzi ukifanywa kwa weledi itatusaidia kudhibiti janga hili kwani wanyama pori wamekuwa chanzo cha virusi kukaa nao wakipata itaondoa hofu kwa watanzania,” aliongeza.

Aidha Chifu Mwariko ambaye ni msanii wa kitaifa na kimataifa na anayejihusisha na masuala ya kimila aliendelea kupongeza juhudi ambazo Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuzichukua kuhakikisha nchi haitetereki katika kipindi hiki ambacho ulimwengu unazidi kutoa machozi.

“Shukrani nyingi zenye furaha na amani tushukuru tumejiwa na mgeni mwema mzuri na tulikuwa tunategemea miaka mingi tupate Rais mama katika nchi yetu ya Tanzania na tumeshapata na tunafurahi na tunaunga mkono sasa. Ni mmoja katika wamama wa aina yake na pia  katika bara la Afrika hata ulimwengu  mzima sisi tunashukuru tumepata kiongozi mwenye busara na mwelewaji kama Mama Samia Suluhu Hassan,” anasema Chifu Mwariko.

Majuma kadhaa yaliyopita Serikali ilieleza kuwa mikoa ya Kilimanjaro na Mwanza imekuwa hatari kwa maambukizi na vifo vya watu walioambukizwa kirusi cha Delta, wimbi hilo la tatu ambalo limezua taharuki dunia.

0 Comments:

Post a Comment