ARUSHA, TANZANIA
Kongamano la siku tisa la Mawasiliano ya Amani (CNVC) limeanza jijini Arusha kwa washiriki kutoka mataifa 13, likijikita zaidi katika kujifunza namna ya kuitengeneza jamii yenye amani na utulivu kwa kuanza na maisha ya ndani ya mtu binafsi.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo Askofu Joseph Laizer wa Kanisa la Christian Life Tanzania, amesema katika dunia ambayo maadili yameporomoka kuna ulazima wa kujifunza utu wa ndani wa binadamu ambao ndio chemichemi ya kujenga jamii iliyo bora.
"Utu wa ndani wa binadamu unaweza kuwafanya watu wengine wasijisikie vizuri hivyo ni muhimu pawepo na makongamano ya kufundisha namna ya kujitambua kwanza kwa ustawi wa jamii," amesema Askofu Laizer.
Askofu Laizer ameongeza kuwa binadamu amekuwa na changamoto nyingi katika moyo wake ambazo zinahitaji neema ya Mungu kupata ufumbuzi.
"Kitabu cha Mhubiri 9:3 kinaeleza kuhusu mahangaiko aliyonayo mtu, lakini hayo yote yanahitaji neema ya Mungu kwa ajili ya kupata ufumbuzi," ameongeza.
Aidha Askofu Laizer amesema wazazi wana wajibu mkubwa wa kuifanya jamii ikawa ya amani na utulivu ikiwa kama nao walipata msingi bora wa malezi.
"Mithali 22:6 inaweka msisitizo juu ya malezi bora ya mtoto ambao ni wajibu wa mzazi husika, kama mzazi hajalelewa katika malezi bora mtoto wake atakuwaje na malezi bora katika kizazi hiki cha utandawazi?" anahoji Askofu Laizer.
Hata hivyo msisitizo umetolewa kwa kila mmoja kutekeleza wajibu wake kwani hakuna mwanadamu aliyeumbwa ambaye hakupangiwa kusudi la kufanya katika dunia.
"Hakuna aliyezaliwa kwa bahati mbaya, ili kuiokoa jamii yetu ni muhimu kila mmoja afanye wajibu wake ikiwamo tamaduni bora kwa watoto wetu," amesema Askofu Laizer.
Kauli mbiu ya Kongamano, "Pamoja tunaweza kutambua lugha na njia mahsusi ya kuyafanya maisha kuwa mazuri, kwa kujifunza kusikiliza mahitaji yetu ya ndani."
Mwenyekiti wa Kongamano hilo Martha Patrick Dello amesema katika siku tisa za kongamano hilo washiriki wataweza kutambua ni kwa namna gani walivyo na umuhimu katika ujenzi wa maisha yao binafasi na jamii inayowazunguka.
"Kwa mara ya kwanza nilipopata semina ya Mawasiliano ya Amani, moyo wangu ulifunguka na niliporudi Tanzania nilitamani kila mmoja ajue kile nilichokuwa nacho, bahati nzuri kila nilipopita katika nyumba, shule walinielewa nikajisikia vizuri,... ni shauku yangu nawe utajifunza," amesema Martha Dello.
Washiriki 78 katika Kongamano hilolililoratibiwa na Intensive International Training (IIT) Tanzania ni kutoka Uganda, Kenya, Ghana, Ubelgiji, Ujerumani, Zimbabwe, Ufilipino, Marekani, Tanzania, Austria, Italia, Hungaria na India.
Chimbuko la Mawasiliano ya Amani
Marshall Rosenberg |
Daktari Marshall Bertram Rosenberg (1934-2015) ndiye mwanzilishi wa Mawasiliano ya Amani (NVC).
Mwanasaikolojia huyu katika malezi yake ya kimaskini na yaliyojaa taabu za kila namna alitaka kujua chanzo na namna ya kupata utatuzi juu ya mateso ya ndani ambayo binadamu amekuwa akiyapata.
Kupitia kitabu chake maarufu, "Non Violent Communication: A language of Life" Dkt. Marshall mpaka sasa amejizoelea wafuasi wengi kote ulimwenguni katika kushughulika na changamoto za ndani za mwanadamu.
Madhumuni makubwa ya Dkt. Marshall haikuwa kumaliza kabisa mateso hayo ila ilikuwa ni kujaribu kupunguza ili kuboresha maisha ya mtu na jamii kwa ujumla.
Tukio la mwaka 1934 huko Detroit, Michigan lililosababisha vifo vya watu 34 na wengine 433 kujeruhiwa liliamsha azma ya Dkt. Marshall ya kuijenga jamii bora alipojiuliza, "Kwanini watu wanafanya hivi, na kwanini haya pia yanatokea kwangu?"
Enzi za uhai wake Dkt. Marshall alikua akitembelea nchi takribani 35 kwa mwaka kwa ajili ya kufundisha kuhusu namna bora ya kuijenga jamii bora yenye amani na utulivu. Dkt. Marshall alifurahia sana mafanikio ya kazi yake.
"Huwezi kuamini mambo yaliyokuwa yanatokea pindi ninapoondoka baada ya kutoa semina, kwani nilipokuwa nikirudi tena ilikuwa vigumu kuamini namna walivyofikia mafanikio kwa muda mwafaka tangu nilipowaacha," mojawapo ya maelezo ya Dkt. Marshall enzi za uhai wake.
Tuzo mbalimbali Dkt. Marshall ametunukiwa ikiwamo tuzo ya Shujaa na Mshindi wa Kusamehe (Hero and Champion of Forgiveness Award)aliyoipata mwaka mmoja kabla ya kifo chake.
0 Comments:
Post a Comment