BIGWA-KISIWANI, MOROGORO
Miaka ya ujana ndiyo miaka inayoumba maisha ya mtu. Katika kujua tabia za vijana, ni muhimu kukumbuka kuwa hakuna vijana wawili walio sawa.
Walakini, vijana wote hupitia mabadiliko ya kifizikia na homoni ambazo zinaweza kuwaumba kuwa watu wazima ambao watakuwa kwenye siku zao za usoni, unaandika mtandao wa AfricaParent katika makala yake kuhusu vijana.
Unapozungumza neno vijana kila mmoja kati yetu atatafsiri kwa maana tofauti lakini wote tutakuwa na ujumbe mmoja.
Wapo watakaosema ni wale watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 45, wengine wangesema ni watu wale wenye uwezo wa kufanya majambo huku damu zikiwachemka na kadhalika.
"Vijana msilale lale lale! Vijana msilale bado mapambano!" Lakini kwanini wawe vijana na wasiwe wazee au watoto? Huenda watunzi wa nyimbo hii walifahamu mengi juu ya vijana na uwezo wa vijana na katika utendaji wa kazi.
Nukta hizo kuhusu vijana zinaligusa moja kwa moja Shirika lisilo la Kiserikali la Highlands 255 lenye kujishughulisha na kuwaunganisha vijana nchini Tanzania.
Highlands 255 iliyopo Bigwa, Kisiwani nje kidogo ya mji wa Morogoro imekuwa ikifanya hivyo kwa takribani miaka 12 tangu kuanza kwake mnamo mwaka 2010.
Ukitazama kwa makini kupitia Hoja za Dkt. Adolf Mihanjo katika kitabu chake cha Falsafa na Usanifu wa Hoja-Kutoka Wayunani hadi Watanzania (Waafrika) Plato ndiye mwanafalsafa aliyeanzisha Asitiria ya Pango.
Asitiria hiyo ina mengi ndani yake ikionyesha ukweli kwamba kuna vitu vinavyodumu na vile vinavyopita.
Vingine ni vivuli na vingine ni vitu halisi, ukweli na vitu visivyobadilika milele yote. Mfano, upendo ni kitu kinachodumu milele yote. Watu wanaopendana wanakuja na kupita, lakini upendo upo pale pale.
Highlands 255 imeonyesha upendo ambao utazidi kudumu katika maisha ya vijana waliopata neema ya kuhudhuria kambi mbalimbali tangu kuanzishwa kwake.
Hata hivyo katika kambi ya mwaka huu iliyofanyika kutoka tarehe 17 hadi 20 Mei katika viunga vya shirika hilo ilitia fora katika kila eneo ikiwamo michezo na mafundisho ya Neno la Mungu.
“Sola Gratia” ilikuwa kauli mbiu ya kambi hiyo iliyowakusanya vijana 500 kutoka Kanda ya Kaskazini yaani mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Kauli mbiu hiyo ikiwa na maana ya “Ni kwa Neema tu” ilisimama siku zote za kambi hiyo ikijikita kwenye kisa cha kweli kilichotokea katika karne ya 9 K.W.K cha mtu aliyefahamika kwa jina la Yona mwana wa Amitai.
Licha ya kwamba taarifa za Yona zilikuja kuandikwa karne nne baada ya kifo chake katika karne ya 8 K.W.K lakini zimekuwa na mafundisho mengi kwa vizazi nenda rudi mpaka sasa.
Akifundisha kabla ya kuanza kwa mashindano kwenye Mwalimu na Msimamizi wa Kambi Samweli Mwakipesile alisema, “Kuna vitu tunavipata katika maisha yetu kutokana na neema. Yona alipata neema kutoka kwa Mungu licha ya kumkimbia lakini bado Mungu anamtafuta Yona na Mungu habadiliki katika mpango wake. Wokovu watoka kwa Bwana.”
Mwalimu huyo aliongeza, “Kuna watu wanajiona bora kutokana na dini zao, rangi zao, vipaji vyao, changamoto walizopitia, elimu zao, wengine hawajasoma mambo hayo yote sio chochote mbele za Mungu.”
Baada ya mahubiri hayo zamu ya soka ikawadia ambapo timu 20 kutoka katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro zilijitupa viwanjani kutafuta mshindi wa taji hilo mwaka huu.
Kundi A liliundwa na Arusha Youth, Malezi Bora, Uzunguni FC, Makange FC na Regar Boys. Kundi B lilikuwa na Young Life, Endumet, Kware, Mshewa na Zinduka. Kundi C lilizileta pamoja Peace Academy, Man 2 Man, Young Boys, Mwanga Sport na Kifaru City. Kundi D lilikuwa na Rangers, Studio FC, Motori, Lyamungo, Black Heroes.
Washindi wa kila kundi walizama nusu fainali Arusha Youth, Endumet FC, Peace Academy na Rangers walitinga hatua hiyo.
Hatimaye fainali ilizikutanisha Endumet FC na Arusha Youth katika mtanange ulioamriwa kwa mikwaju ya penati baada ya muda wa kawaida kumalizika.
Endumet FC iliibuka bingwa wa michuano hiyo baada ya kuizabua Arusha Youth kwa mikwaju 4-3.
Kikosi cha ushindi cha Endumet FC katika mashindano hayo kiliundwa na mlinda mlango Adam James aliyeibuka mchezaji bora wa mashindano hayo na kuzawadia tuzo hiyo mbele ya washiriki wote Mei 19, 2022.
Wengine ni Samson John, Nuhu, Edwin Daudi, Ndele Solomon, Rashidi Athuman, Sheyo Michael, Godfrey Emmanuel, Joachim Epimarck, Paulo James na Gerald Alfred.
Said Juma, Rashid Ally, Ramadhan Idrissa, Alan Joseph, Musa Abushehe, Joseph Stephano, Hamad Christopher walifanikisha ushindi huo mwaka huu.
Licha ya kufurahi katika mabwawa ya kuogelea, wakati wa usiku ulikuwa mzuri pia pale maigizo, acrobatics, na dance yaliyobeba ujumbe wa mwaka huu yakifunika mashindano hayo hususani igizo la Kipwipwi Gahawa ambalo liliwavutia sana vijana waliouhudhuria kambi hiyo.
Aidha Mwinjilisti kwa vijana na mhudumu wa Highlands 255 Burton Peter aliwataka vijana kuachana na tabia ambazo zitawaweka mbali na Mungu hivyo kukosa kila kitu katika ulimwengu huu na ule ujao.
Kwa upande wake Mratibu wa Kambi hiyo mwaka huu Mchungaji Cyril Mushi wa kanisa la Baptist alisema, “Mwenyezi Mungu ni mlinzi wa wale walioamini. Huwatoa katika giza na kuwaingiza katika mwanga. Mashindano haya yamenoga kila upande yawe mwangaza kwa kila kijana atakaporudi nyumbani.”
0 Comments:
Post a Comment