Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro Biochem Ltd Shivam Patel
akikabidhi kompyuta kwa Mkuu wa shule ya sekondari ya Kileo Ezekiel Josam
katika hafla iliyofanyika Juni 14, 2022
KILEO, KILIMANJARO
Kampuni ya Uzalishaji wa Spiriti (Kilimanjaro Biochem Ltd)
mkoani Kilimanjaro imetoa kompyuta 20 kwa shule mbili za sekondari wilayani
Mwanga ikiwa ni sehemu ya kuisadia jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa shule za sekondari za Kileo na Mandaka
Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro Biochem Ltd Shivam Patel amesema,
“Tangu tulipoanza kiwanda hiki jukumu letu tuliona ni
kusaidia jamii, kwa hiyo tuliona kutoa kompyuta kwa wanafunzi itawasaidia
kupata taarifa kutoka kwenye mtandao na pia ujuzi mbalimbali ambao utawasaidia
katika maisha yao ya baadaye…jambo la msingi wazilinde ili zitumike kwa muda
mrefu.”
Diwani wa Kata ya Kileo Kuria Msuya amesema juhudi za
viongozi kutafuta wadau wa maendeleo ndio chachu ya mafanikio kwa jamii na
huongeza imani kwa wananchi.
“Niseme tu kwamba mojawapo ya vitu ambavyo vinatufanya
wananchi waone viongozi wanapambana kwa ajili yao ni kutafuta wadau wa
maendeleo na wadau hawa wanapotekeleza zile ahadi au mahitaji ya wananchi
uongozi wako unaoonekanani uongozi shiriki,” amesema Diwani Msuya
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kileo Ezekiel Josam amesema
changamoto iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu imepata ufumbuzi na kwamba
taaluma katika shule itaboreshwa kutokana na zama za utandawazi zilizopo kwa
sasa.
“Tangu shule yetu ilipoanzishwa mwaka 2006 haikuwahi kuwa na
kompyuta mpaka mwaka 2019 tulipata moja; wakaleta na photocopy machine ambayo
ilitusaidia kupunguza gharama. Ujio wa kompyuta hizi ni pamoja na mtandao.
Wadau walikuja na suala la maji lakini nikawaambia tuna uhitaji wa kompyuta
ndio Kilimanjaro Biochem wametuletea. Uchumi wa kati unahitaji maarifa ya
kompyuta na mtandao,”
Aidha Afisa Elimu Taaluma kwa Shule za Sekondari wilayani
Mwanga Emmanuel Kipele ametoa shukrani zake za dhati kwa wadau hao wa maendeleo
“Tuna furaha kupokea msaada wa kompyuta 20 pamoja na
projector mbili kwa ajili ya shule zetu za Kileo na Mandaka…kwa ujumla kompyuta
zitatusaidia katika kuboresha ufundishaji ikiwa ni nyenzo mojawapo ya
kufundishia. Tuna changamoto kubwa ya vifaa vya kufundishia kwa hiyo msaada huu
utatufanya sisi kuendelea kuboresha taaluma katika shule zetu za sekondari,”
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa shule hizo wamesema ulimwengu waliopo kompyuta ni suala lisiloweza kuepukika kutokana na ukuaji wa kasi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
“Zitatusaidia mambo mengi ikiwemo kukuza uelewa wetu,
kujiendeleza kielimu. Mitandao ya kijamii imekuwa ikituathiri sana japokuwa sio
wote kutokana na wanapoenda wanaangalia mambo ambayo yapo nje ya masomo,” Mwanfaa
Abubakar Iddi
0 Comments:
Post a Comment