Monday, June 13, 2022

Kilimanjaro yakabidhi Mwenge Manyara, miradi ya sh. 855milioni yatakaliwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Steven Kigaigai akiukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere katika hafla iliyofanyika Mererani Juni 13, 2022 baada ya kumaliza safari yake mkoani Kilimanjaro ulikopitia miradi 38.

MERERANI, MANYARA

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Steven Kigaigai ameukabidhi Mwenge wa Uhuru katika mkoa wa Manyara baada ya kuukimbiza katika wilaya saba za mkoa wake kwa siku saba ukifungua, ukikagua na ukifungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 38.

Akiwasilisha ripoti yake wakati wa hafla ya kuukabidhi Mwenge wa Uhuru mkoani Manyara iliyofanyika katika Mererani Juni 13 mwaka huu Kigaigai amesema “Katika miradi hiyo miradi 11 ilikuwa ya kufunguliwa, kuzinduliwa na miradi 15 ya kuwekewa mawe ya msingi na miradi 12 ilikuwa ya kukaguliwa.”

Aidha Kigaigai amesema miradi yenye thamani ya shilingi 855, 993,127 haikuzinduliwa kutokana na sababu mbalimbali

“Zilizobainishwa kwa kila mradi ikiwamo moja kutokuwepo kwa nyaraka katika eneo la miradi na hivyo vigumu kufanya ukaguzi kufuatia maelezo ya serikali lakini pili ilikuwa ni utekelezaji wa miradi kutolingana na thamani ya fedha zilizotumika, tatu baadhi ya miradi ilikuwa imetekelezwa nje ya muda uliokubalika kimkataba…, nne  baadhi ya miradi kutozingatia utaratibu wa uidhinishaji wa fedha,” amesema Kigaigai.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Steven Kigaigai akiwasilisha ripoti ya Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere mnamo Juni 13, 2022 wakati akiukabidhi mkoani humo.
Kilimanjaro ilipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Tanga mnamo Juni 6 katika kijiji cha Bendera wilayani Same na ulikimbizwa umbali wa kilometa 853.5 ukizindua, ukikagua mradi 38 yenye thamani ya shilingi 13,670,634,422.60

Mwenge wa Uhuru ulipitia Same ambako ulizindu na kukagua miradi minne, Mwanga miradi sita, Rombo miradi sita, Moshi Vijijini miradi sita, Moshi Manispaa miradi mitano, Hai miradi mitano na Siha miradi sita.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati akitoa hotuba ya Siku ya Uhuru Desemba 9, 1961 aliwatangazia Watanganyika, Afrika na Dunia kwa ujumla akisema, “ Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipojaa dharau.”

Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni, “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo, Shiriki kuhesabiwa tuyafikie Maendeleo ya Taifa.”

0 Comments:

Post a Comment