Mkurugenzi wa Taasisi ya Sanaa ya Kilimanjaro
Cultural Heritage Centre Chifu Athumani Omary
Mwariko ‘Mhelamwana’
Kutokana
na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sanaa ya Kilimanjaro
Cultural Heritage Centre Chifu Athumani Omary
Mwariko ‘Mhelamwana’ amependekeza kuchapishwa kwa noti mpya.
Akizungumza na mwandishi wetu Chifu Mwariko alisema, wakati umefika wa kutengeneza noti mpya ambayo itakuwa na picha ya Rais Samia ikiwa ni kumbukumbu ya taifa kuwa na kiongozi wa kwanza mwanamke katika nafasi hiyo.
“Mimi kama msanii katika fani ya sanaa tumeona ipo haja ya kumpongeza na kumpa zawadi ambayo ni kutengeneza noti mpya itakayokuwa ikitumika ulimwengu mzima kuhusiana na yeye kama mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania,” alisema.
Chifu Mwariko alisema Rais Samia amejitahidi kwa kiasi kikubwa ndani ya muda mchache kuifanya nchi kuwa sehemu salama hata kama kuna changamoto za hapa na pale.
Aidha chifu huyo maarufu nchini kwa mapendekezo mbalimbali ya namna ya kuijenga nchi aliongeza kuwa ziara ya Rais Samia ya Royal Tour imeliongezea taifa heshima hivyo katika noti mpya kuwepo na neno ‘The Royal Tour”.
“Kupitia filamu ya Royal Tour tunayo nafasi ya kila mmoja wetu kumpongeza Rais Samia kwa uzalendo ambao ameuonesha kwa taifa letu na vijana wa nchi hii tutaendelea kumuombea maisha marefu na afya njema,”aliongeza Chifu Mwariko.
Mnamo mwaka 2020 Chifu Mwariko alitoa mapendekezo ya Mlima Kilimanjaro kuwekewa pazia ili kuweka mazingira mazuri ya kukusanya mapato kutokana na sekta ya utalii kuwa namba moja kuiletea Tanzania mapato kwa wingi.
Pia mwaka huo huo Chifu huyo alipendekeza ichapishwe noti ya shilingi 50,000 ya Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli.
0 Comments:
Post a Comment