Tuesday, June 28, 2022

ACP Maigwa: Ajali zinaepukika

Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro (ACP) Simon Maigwa

Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, limewataka madereva mkoani humo kujali, kufuata taratibu, kanuni  na sheria za usalama barabarani  ili kuepusha ajali.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya elimu ya usalama barabarani kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto yaliyofanyika katika shule ya msingi Sanja Juu wilaya ya Siha mkoani humo, Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro (ACP) Simon Maigwa, alisema “Ni vema kila dereva  akatambua amebeba roho za watu hivyo akafuata sheria zote za barabarani ili kuepusha ajali kwani ajali inapotokea inapoteza roho za watu pia inapunguza nguvu kazi ya taifa”.

ACP Maigwa alisema chanzo kikubwa cha ajali nyingi za usalama barabarani zinachangiwa na makosa ya kibinadamu, kwa kutokuzingatia sheria, kanuni za usalama barabarani ikiwemo mwendo kasi, ulevi, na upakiaji wa hatari.

“Changamoto kubwa tuliyonayo katika mkoa wetu wa Kilimanjaro ni matukio ya ajili za barabarani zinazosababishwa na madereva wa pilkipiki na kusababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi wanaopata ulemavu wa kudumu,”alisema.

Alisema wapo baadhi ya madereva wa bodaboda ambao hawana taaluma hiyo, hali ambayo inachangia kuwepo kwa ajali nyingi, na kuwataka madereva wanaoendesha vyombo  vya moto kuwa makini na kufuata  sheria za usalama barabarani kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kutokuwepo kwa ajali.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Usalama barabarani mkoa wa Kilimanjaro (SSP) Pili Misungwi, alisema mafunzo hayo yalikuwa ni kuwakumbusha madereva na wamiliki wa vyombo vya moto, jinsi ya kufuata sheria za barabarani na kuendesha gari kwa mwendo ambao unatakiwa ili kuepusha ajali na kuokoa maisha ya wananchi.

“Madereva  wengi wa pikipiki wamekuwa wakiendesha vyombo vya moto bila kupata mafunzo ya sheria za usalama barabarani, wamekuwa ni miongoni mwa visababishi vikubwa vya ajili zinazotokea katika mkoa huu,”alisema SSP Misungwi.

Kwa upande wake Mkufunzi wa elimu ya udereva kutoka chuo cha Winners kilichopo Bagamoyo Pastory Patrick,  alisema lengo la mafunzo hayo ni kutokana na madereva wengi  waishio maeneo ya vijijini kukosa uelewa wa sheria za usalama barabarani wakati wakiendesha vyombo vya moto ikiwamo ukosefu wa mafunzo ya udereva.

Daniel Twain na Joseph Omary ni miongoni mwa madereva 65 kati ya 117 waliohitimu mafunzo, wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa mafunzo hayo, kwa sababu yamewakumbusha kufuata sheria za barabarani, kutokana na kwamba wengi wanafanya kazi hiyo kwa mazoea.



 

0 Comments:

Post a Comment