Sunday, June 12, 2022

Wanaharakati wataka sheria kali kudhibiti ukatili wa watoto

Wito umetolewa kwa serikali kulivalia njuga suala la watoto kufanyiwa ukatili ikiwamo kutunga sheria zinazotekelezeka kwa wahusika wanapobainika kutenda vitendo hivyo kutokana na kukithiri kwa matukio hayo.

Akizungumza na vyombo vya habari David Msuya, mwanaharakati wa haki za watoto wanaosoma mashuleni barani Afrika amesema kesi zimekuwa zikichukua muda mrefu jambo ambalo limekuwa likififisha juhudi za kupunguza ukatili huo.

“Kila siku kumekuwa na matukio ya mauaji, tunaiomba serikali kutunga sheria, sheria hii iwe na meno kwa maana mtu akishtakiwa kesi hizi zisiwe zinachukua muda mrefu, tumeshaona watoto wadogo wanalawiti mashuleni, walemavu wanafichwa majumbani…” amesema Msuya

Msuya ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Elimu cha Furahika kilichopo jijini Dar es Salaam amesema sheria inatakiwa kuchukua mkondo wake pasipo kuangalia uwezo na hadhi ya mtu.

Hata hivyo amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kugundua familia ambazo zimekuwa na watoto waliopo kwenye mazingira magumu sio mpaka wafuatwe.

Aidha Msuya amesema mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Tabora, Shinyanga, Mtwara na Ruvuma  inaongoza kwa kuwa matukio ya watoto kufanyiwa ukatili.

Mwanaharakati wa haki za watoto wanaosoma mashuleni barani Afrika David Msuya akiitaka serikali kusimamia sheria dhidi ya wanaothibitika kufanya ukatili kwa watoto. 

SHERIA YA MTOTO YA MWAKA 2009

Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 inashughulikia haki za watoto Tanzania. Sheria hii inajumuisha mambo mbalimbali ya kukuza, kulinda, na kuhifadhi ustawi wa mtoto; masharti ya unajibishaji wa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa; masuala ya kulea, kuasili na uangalizi.

Mtoto anaweza kufanyiwa vitendo kama: kutelekezwa au kutopatiwa matunzo na wazazi/walezi, kupigwa, kubakwa, kulawitiwa, na kupewa ujauzito. Watoto wanahitaji ulinzi kwani vitendo hivi vingi huanzia majumbani. Ni muhimu wazazi kujua kuwa vitendo hivi wanavyofanyiwa watoto ni uvunjaji wa sheria.

WAJIBU WA AFISA WA USTAWI WA JAMII

1.  Afisa ustawi wa jamii ana wajibu wa kufuatilia kituoni kuona kama kuna watoto watuhumiwa.

2.  Ana wajibu wa kuwasiliana na Askari polisi juu ya shauri lolote linalomuhusu mtuhumiwa ambaye ni mtoto.

3.   Pia ana wajibu wa kulinda maslahi ya mtoto katika mfumo huo wote na kuhakikisha haki zake zinazingatiwa.

 

0 Comments:

Post a Comment