Friday, June 10, 2022

Wananchi Siha watakiwa kujitokeza kupima Kifua Kikuu

Wananchi kushindwa kutambua dalili za ugonjwa wa kifua kikuu imekuwa changamoto kubwa na kusababisha ugonjwa huo kuenea kwa kasi katika maeneo ya vijijini.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni maalum ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro Dkt. Daniel Matatizo amesema mwitikio wa wakazi wa eneo hilo kupima upo chini hali ambayo inaweza kuwa hatarishi.

“Baada ya kuona uibuaji na upimaji wa kifua kikuu uko chini, tumeamua kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa kushirikiana na Hospitali ya Kibong’oto  pamoja na Mkuta kwa muda wa siku kumi,” amesema Dkt. Daniel

Kaimu mganga mkuu huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha amesema wamefanikiwa kuwagundua watu wenye dalili za ugonjwa huo wapatao 37 huku watatu kati yao wakiwa na kifua kikuu sugu.

“Tumetembelea kaya 23 na makundi mbalimbali sita ikiwemo vijiwe vya bodaboda, mikutano ya hadhara na tumeweza kuona takribani 600 watu tumeweza kuwafikia, kuwapa eklimu ya kifua kikuu kati ya hao tumeweza kubaini wahisiwa wa ugonjwa wa kifua kikuu 37 na kati ya hao tumeweza kugundua wagonjwa watatu kifua kikuu sugu, ambao tayari tumewaanzishia matibabu,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Siha Thomas Apson, amesema kampeni hiyo imekuwa bora na yenye matokeo chanya badala ya watalaamu hao kusubiri kufuatwa hospitali wameamua kuifuata jamii ili kuepusha maambukizi mapya.

“Tuna ugonjwa huu hatarishi ambao wananchi wengi wanatakiwa kuufahamu, na njia mojawapo ya kuuwahi ugonjwa huo ni vizuri mkajitokeza mkapima, na mliokuwa hamjijui mkiishi kawaida, tayari mtaanza kupata matibabu bure,” amesema Mkuu wa Wilaya huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Siha Thomas Apson akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya kupima Kifua Kikuu 

Tanzania ni kati ya nchi 30 zenye viwango vikubwa vya maambukizi ya Kifua kikuu duniani.

Kifua kikuu husababishwa na bakteria aitwaye Mycobacterium. Ikiwa unawasiliana na mtu aliyeambukizwa, kupiga chafya, kukohoa na kuenea kwa hewa kunaweza kuambukiza watu wanaozunguka. Viini vya kifua kikuu vinaweza kuenea hewani hata kutoka kwa maneno.

Kohozi la mtu linapoachwa mahali penye kivuli, vijidudu huishi kwa muda mrefu. Unaenea zaidi katika vyumba vichafu, vilivyofungwa, visivyo na hewa. Ikiwa kuna watu zaidi katika chumba kimoja, huenea kwa kasi.

0 Comments:

Post a Comment