Saturday, June 11, 2022

Mradi wa Maji Kikafu Soka wapokea hati ya pongezi

 

Watumishi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) mkoa wa Kilimanjaro katika picha ya pamoja baada ya kukabidhi kwa hati ya pongezi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Nyanzabara Geraruma kutokana na utendaji wao mzuri kwenye Mradi wa Maji wa Kikafu Soka-Hai Mjini.

HAI, KILIMANJARO

Mradi wa Maji wa Kikafu Soka wilayani Hai umepewa pongezi nyingi na Mwenge wa Uhuru baada ya kukamilika kwake unatarajiwa kuondoa kero ya maji iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa Bomang’ombe na maeneo ya karibu.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu Sahil Nyanzabara Geraruma amesema mradi huo una uwezo mkubwa wa kufuta kabisa kero ya maji kwa wakazi wa Hai Mjini.

“Mkandarasi tengeneza mazingira rafiki na waliokupa kazi, maliza kwa wakati…weka umeme ili wananchi hawa wanufaike na mradi huu,” amesema Geraruma.

Katika ripoti ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) mkoa wa Kilimanjaro kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru inasema mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Helpdesk Engineering (T) Ltd tangu Desemba 29, 2021 na utakamilika Agosti 29, 2022.

Meneja wa Ruwasa mkoa wa Kilimanjaro Weransari Munis amesema mradi huo unatumia chanzo cha chemichemi ya Kikafu Soka kilichopo katika kijiji cha Kimashuku kata ya Mnadani.

“Chemichemi ya Kikafu Soka ina uwezo wa kuzalisha wastani wa lita za ujazo 100 kwa sekunde kwa sasa mradi unachukua kiasi cha maji cha wastani wa lita za ujazo 25 kwa sekunde na mita za ujazo 2,160 kwa siku. Hii itaondoa upungufu wa maji kwenye maeneo hayo kwa asilimia 100,” amesema Munis.

Mradi wa Kikafu Soka unatekelezwa kwa fedha za serikali kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF) kwa kiasi cha shilini bil. 3.3 na utekelezaji wake umefikia asilimia 43 hadi sasa.

Wakazi 55,855 watanufaika na mradi huo hivyo kuondoa tatizo kubwa la maji katika kata za Bomang’ombe, Muungano na Bondeni na kuongeza kasi ya Mji wa Hai kimaendeleo.

Meneja wa Ruwasa mkoa wa Kilimanjaro Weransari Munis akipokea maelekezo kutoka kwa viongozi wa mbio za mwenge kwenye chanzo cha maji cha Kikafu Soka

Mwenge wa Uhuru uliopowasili katika kijiji cha Kimashuku kwa ajili ya kukagua mradi wa maji wa Hai Mjini

Chanzo cha Maji cha Kikafu soka katika ujenzi ili kutatua changamoto ya maji kwa wakazi wa Hai Mjini.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Nyanzabara Geraruma akizungumza baada ya kuridhishwa na mradi wa maji wa Hai Mjini


1 comment: