Mkurugenzi wa Chuo cha Udereva Wereni kilichopo mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro Reuben Mush akizungumza na wahitimu wa kozi ya udereva
Wito umetolewa kwa mamlaka zinazohusika na utoaji wa leseni za udereva kuwapima afya wanafunzi wao ili kupunguza vifo na majeruhi vinavyotokana na ajali za barabarani.
Hayo yanajiri baada ya uchunguzi wa muda mrefu kuhusu vyanzo vya
ajali mbalimbali nchini ambapo zimekuwa zikitokana na madereva
kupewa leseni za vyombo vya usafiri bila kufanyika uchunguzi wa afya
zao.
Mkurugenzi wa Chuo cha Udereva Wereni kilichopo mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro Reuben Mushi, ameyasema hayo Juni 27,2022 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wiki moja ya usalama barabarani kwa maaskari magereza wa gereza la Karanga mkoani Kilimanjaro.
“Kuwa baadhi ya watu
wana ugonjwa wa kifafa lakini kutokana na kwamba hauonekani kwa macho wanakuja
na kuomba leseni, anaweza akaugua au ukamjia wakati akiendesha chombo cha moto
na kusababisha ajili na vifo, tunashauri ni vizuri wataalamu wa masuala ya afya
wawepo wakati wakitoa leseni hizo ili waweze kupimwa kabla ya kupatiwa
leseni,”amesema.
Amesema Jeshi la
Polisi kitengo cha Usalama Barabarani wenye dhamana ya kutoa leseni za udereva
wanalojukumu la kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaofika kuomba kupatiwa leseni
ni vizuri wakawa wanawashirikisha wataalamu wa afya ya akili ili waweze
kuwapima kwani baadhi ya waombaji wa leseni hizo ni wagonjwa wa akili.
Amesema lengo la
mafunzo hayo ya usalama barabarani kwa madereva ambao ni maaskari magereza, ni
kutokana na kutokuwa na muda wa kufika darasani kutokana na kuwa na majukumu
mengi ya kikazi.
Kwa niaba ya Mkuu wa
gereza la Karanga Moshi, Inspector Francis Gweba, amekishukuru chuo cha udereva
cha Wereni kwa kuona umuhimu wa kuwafikia na kuweza kutoa elimu ya
usalama na kwamba wao kama maaskari watakuwa kioo katika jamii katika kusimamia
sheria za usalama barabarani na wasiwe kikwazo katika kuvunja sheria
hizo za usalama barabarani.
Baadhi ya washiriki wa
mafunzo hayo wamesema wengi wao wana vyombo vya moto hawana elimu inayohusiana
na masuala ya usalama barabarani hivyo elimu hiyo imekuwa fursa kwao kuweza
kuzitambua sheria na kanunia za usalama barabarani.
Mkaguzi msaidizi wa Jeshi la Polisi Maneno Francis kutoka Ofisi ya Usalama Barabarani (RTO) mkoa wa Kilimanjaro, kitengo cha Elimu kwa Umma,
Kwa upande wake Mkaguzi msaidizi wa Jeshi la Polisi Maneno Francis kutoka Ofisi ya Usalama Barabarani (RTO) mkoa wa Kilimanjaro, kitengo cha Elimu kwa Umma, amesema kwa kushirikiana na chuo cha udereva Wereni kutoa elimu kwa wananchi wa Magereza lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu ya usalama barabarani.
“Katika vyanzo vikuu
vitatu vya ajali za barabarani, zinachangiwa na makosa ya
kibinadamu, ubovu wa vyombo vya moto, pamoja na miundombinu na hali ya hewa, makosa ya kibinadamu
yanachangia kwa asilimia 80, ubovu wa vyombo vya moto asilimia 12 huku miundombinu
na hali ya hewa inachangia kwa asilimia 8,” amesema.
0 Comments:
Post a Comment