Tenki la Maji la Mradi wa Njoro II lililopo katika kijiji cha Nanjara wilayani Rombo baada ya kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru mnamo Juni 8, 2022 na Kiongozi wa mbio hizo Sahil Nyanzabara Geraruma. |
ROMBO, KILIMANJARO
Wakazi wa tarafa za Tarakea, Userri na Mashati wapo mbioni kuondokana na changamoto ya maji baada ya mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 667 kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru.
Akiwasilisha mbele ya Kiongozi wa Mwenge kitaifa Afisa Uhusiano Selestine Mtenga amesema Wakala wa Maji Safi na Salama mkoa wa Kilimanjaro umetekeleza mradi huo kutokana na shida kubwa ya maji iliyopo kwenye ukanda wa chini wa tarafa ya Tarakea.
“Mradi huu unajulikana kama Mradi wa Maji Njoro II upo katika kijiji cha Nanjara, umetekelezwa kutokana na shida kubwa ya maji iliyopo kwenye vijiji vya ukanda wa chini wa Tarafa ya Tarakea,” amesema Mtenga.
Mtenga ameongeza kuwa vyanzo vya mradi huo vipo katika msitu wa Rongai Kata ya Motamburu Kitembeni umbali wa kilometa 17 hadi kwenye tenki la maji.
“Wakazi wapatao 24,686 katika vijiji 15 vya tarafa za Tarakea, Usseri na Mashati watanufaika na mradi huu ambao utazalisha mita za ujazo 1728 kwa siku na kwamba utakuwa umewatua kina mama ndoo kichwani na pia utachochea kazi ya maendeleo na kuinua pato la taifa kwenye vijiji vilivyolengwa,” amesema.
Hata hivyo Mtenga ameweka bayana kuwa vijiji vingine tisa vilivyoko kwenye Tarafa za Usseri na Mashati vitanufaika na mradi huo baada ya serikali kupitia Ruwasa kutenga kiasi cha shilingi milioni 667,102, 258 ambazo ni fedha za Uviko-19.
“Hadi sasa mkandarasi amekamilisha kwa asilimia 50 na anatakiwa awe amekamilisha na kiukabidhi ifikapo tarehe 30 Juni 2022 na mkakati uliopo ni kuendeleza kwenye vijiji vingine tisa vilivyopo kwenye tarafa za Usseri na Mashati,” amesisitiza Afisa Uhusiano huyo.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahil Nyanzabara Geraruma amesema
“Mradi wa
maji ni mzuri, fedha zilizotumika zimeendana na thamani ya mradi, hongereni kwa
Ruwasa kwa kusimamia vizuri fedha za mapambano ya Uviko-19, Mwenge wa Uhuru umeridhika
kuweka jiwe la msingi katika mradi huu. Tayari kwa matumizi kwa wananchi wa
maeneo haya,” amesema Geraruma.
Baadhi ya wakazi wa Tarafa za Tarakea, Usseri na Mashati wametoa pongezi zao kwa serikali kwa kuiona changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili kwa miaka mingi.
Godwin Mshangila amesema, “Kwa wilaya ya Rombo toka mwaka 1990 changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama ilikuwa kubwa sana, baada ya kuingia Kili Water na baadae RUWASA changamoto ya maji imepungua kabisa. Akina mama walikuwa wanaamka saa tisa za usiku kwenda kutafuta maji na kurudi saa nne asbuhi, hali ambayo ilikuwa inaleta kero kubwa ndani ya familia.”
Rozalia Rudovick amesema, “Tulikuwa tukienda mtoni kuchota maji, tunatoa shukrani sana kwa rais samia sulu Hassan kwa kuweza kutoa fedha na kujenga miradi ya maji ambayo imetupunguzia nadha ya kutembea umbali kutafuta maji.”
0 Comments:
Post a Comment