Thursday, June 30, 2022

Upikaji gongo vyanzo vya maji uchafuzi wa mazingira


Upishi wa Gongo

Uongozi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) Kanda ya Kaskazini, umesikitishwa na kitendo cha baadhi ya watu wanaojishughulisha na upikaji wa pombe ya kienyeji aina ya Gongo kwenye nyanzo vya maji na kumwaga uchafu huo kwenye vyanzo hivyo.

Akizungumza kwenye semina iliyowashirikisha madiwani, viongozi wa serikali za mitaa na kata, pamoja na viongozi kutoka Manispaa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MUWASA), kikao kilicxhofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bonde la Pangani mjini Moshi Afisa Mazingira Bonde la Pangani Mhandisi Arafa Maggidi alisema kitendo hicho kimekuwa mwiba kwa baoanuai kwenye vyanzo vya maji.

Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) Injinia  Segule Segule, Injinia Maggidi alisema changamoto nyingine ni watu kupuuza sheria ya mazingira kwani wamekuwa wakifanya ujenzi ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji, kutiririsha maji taka moja kwa moja ndani ya vyanzo vya maji na kuchimba mchanga na mawe ndani ya vyanzo hivyo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watuamia Maji mto Rau Habibu Lema, alisema utoaji wa vibali  holela vya ujenzi vya makazi kutoka Manispaa ya Moshi umechangia kwa kiasi kikubwa watu kujenga karibu na vyanzo vya maji.

“Utoaji wa vibali  vya ujenzi vya makazi kutoka Manispaa ya Moshi umechangia kwa kiasi kikubwa watu kujenga karibu na vyanzo hivyo vya maji,”amesema Lema.

Naye Mjumbe wa Watumia maji Teresia_Mlay, ameupongeza uongozi wa Bonde la Pangani kwa kuanza kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji jambo ambalo limesaidia kupunguza uharibifu wa vyanzo vya maji uliokuwepo.

“Tunashukuru Bonde la Pangani kwa kuanza kuwaelimisha watu na wananchi wameipokea elimu hiyo sasa hivi wameanza kutekeleza maagizo ambayo yamekuwa yakitolewa na wataalamu hao,”amesema Bi. Teresia.

Bodi ya Maji Bonde la Pangani wako katika maadhimisho ya wiki ya Bonde la Pangani kuandia Juni 25 hadi Julai 2, mwaka huu kwa kufanya usafi kwenye Vyanzo vya Maji, kutembelea vituo vya watu wenye mahitaji maalumu pamoja na kuonesha shughuli mbalimbali za kazi zinazofanywa na Bonde hilo.

 

0 Comments:

Post a Comment