Tuesday, June 28, 2022

Bwawa la Nyumba ya Mungu lapendekezwa kufungwa

 

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Steven Kagaigai akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mwanga

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Steven Kagaigai, amesema kutokana na kukithiri kwa uvuvu haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, atamshawishi Waziri wa Mifugo na Vvuvi Mashimba Ndaki, kufunga Bwawa hilo kwa mwaka mmoja.

Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa juma, kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, kilichopitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Uamuzi wa kufunga Bwawa hilo linalotegemewa na Wananchi wa vijiji vya wilaya za Mwanga na Moshi   mkoani Kilimanjaro na Simanjiro mkoa wa Manyara, ulitokana na taarifa ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Mwanga Jafari Kandege.

Kandege katika taarifa hiyo, alisema kwa sasa samaki wanaovuliwa kwenye Bwawa hilo ni wadogo, hali inayosababisha kupungua ukusanyaji mapato katika halmashauri hiyo.

"Wilaya ya Mwanga imejengwa na Bwawa la Nyumba ya Mungu, huko nyuma kulikuwa na mapato makubwa yaliyotokana na samaki katika Bwawa hilo, kwa sasa halmashauri ya Mwanga inapoteza mapato mengi sana, kwa sababu ya uvuvi haramu katika Bwawa hilo,"amesema Kandege.

Aidha Kandege alishauri Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) kufika katika Bwawa hilo kwa haraka na kufanya tathmini, ili kuanzisha uvuvi utakaokuwa ukitumia vizimba kama inavyofanyika Ziwa Victoria, jambo litakalowezesha kupunguza changamoto ya uvuvi haramu na kupata mapato mengi zaidi.

Akizungumza katika kikao hicho kilichokutanisha pia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, Mkuu wa mkoa alimwagiza Kamshina Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro (ACP) Simon Maigwa, kutengeneza mkakati wa pamoja katika pande zote mbili za Kilimanjaro na Manyara ili kukutana na kujadili namna ya kukabiliana na changamoto ya uvuvi haramu kwenye bwawa hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mwanga Mwajuma Nasombe, amesema halmashauri hiyo wanategemea zaidi kukusanya mapato yake kutoka katika vyanzo vikuu viwili.

"Asilimia 50 ya mapato yetu tunakusanya kutoka kwenye madini ya ujenzi, huku asilimia 20 ikitokana na makusanyo kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Ameongeza kusema kuwa “Baada ya Bwawa hilo kughubikwa na uvuvi haramu, mapato yameshuka sana na kuiomba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kuweka nguvu zaidi katika kusaidia uvuvi huo haramu, amesema Bi. Mwajuma.


 

 

0 Comments:

Post a Comment