Machi 3, 2017 alifariki dunia msomi na mwanasiasa wa Haiti René Garcia Préval.
Preval alistaafu masuala ya siasa na kujikita katika miradi ya kilimo huko Marmelade.
Mara ya mwisho alionekana katika hadhira Februari 7, 2017 wakati wa kumtambulisha Jovenel Moise ambaye alishika dola kuanzia hapo hadi sasa.
Rais Moise alitangaza kifo cha Preval Machi 3, 2017 katika akunti ya twitter. Ndugu, jamaa na marafiki wa familia walisema Preval alifariki dunia katika hospital huko Port-au-Prince.
Chanzo cha kifo chake kilitajwa kuwa ni shambulio la moyo licha ya kuwepo kwa taarifa kuwa kiharusi ndio kilimuondoa duniani kiongozi huyo.
Mwili wa Preval ulihifadhiwa katika makaburi ya Mashujaa yaliyopo Champ de Mars, baada ya ibada iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Kiosque Occide Jeanty.
Marais wa zamani wa taifa hilo Jocelerme Privert, Michel Martelly na Prosper Avril walihudhuria mazishi hayo pia ujumbe wa kimataifa ulikuwapo katika mazishi. Preval alizikwa kwa heshima zote za kitaifa kwa kupigiwa mizinga mitatu.
Alikuwa Rais wa taifa la Haiti katika vipindi viwili kutoka Februari 6, 1996 hadi Februari 7, 2001.
Pia Preval alirudi tena kushikilia wadhifa huo kutoka Mei 14, 2006 hadi Mei 14, 2011.
Kabla ya hapo alishawahi kuwa waziri mkuu wa Haiti kutoka Februari 1991 hadi Oktoba 11, 1991.
Préval ndiye rais wa kwanza kwenye historia ya Haiti kuchaguliwa katika hali ya amani tangu kupata uhuru wa taifa hilo.
Pia Préval aliweka rekodi ya kuwa wa kwanza kuliongoza taifa hilo kwa vipondi viwili tofauti. Aidha Préval aliweka rekodi ya kwanza ya kuwa waziri mkuuu aliyechaguliwa kuwa Rais.
Enzi za utawala wake alikuwa akihamasisha ubinafsi wa mashirika ya serikali, mapinduzi ya kilimo na utafiti kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu.
Licha ya kupambana kuutengeneza uchumi wa taifa hilo lakini mnamo mwaka 2010 kulishuhudiwa uharibifu mkubwa uliotokana na tetemeko la ardhi lililoteketeza miundombinu maidhubuti iliyowekwa na kuimarishwa kwa kiasi kikubwa na Preval.
Préval alizaliwa Januari 17, 1943 huko Port-au-Prince na kukulia katika mji amabao baba yake alizaliwa wa Marmelade katika kijiji cha Artibonite.
Aliingia darasani na kusomea masuala ya kilimo katika chuo cha Gembloux na baadaye katika Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji.
Pia alisomea sayansi ya nishati itokanayo na joto la ardhi katika Chuo Kikuu cha Pisa huko nchini Italia. Aliondoka Haiti na familia yake mnamo mwaka 1963.
Baada ya miaka mitano ya kuishi kwake nchini Marekani huko Brooklyn jijini New York, Préval aliamua kurudi Haiti. Alipokuwa nchini Marekani alikuwa akifanya kazi kama mhudumu wa mgahawa.
Aliporudi nchini Haiti alipata nafasi kwenye Taasisi ya Taifa ya Madini.
0 Comments:
Post a Comment