Monday, March 2, 2020

Taasisi ya Kijana Kwanza yatoa madawati 100 Reginald Mengi Secondary School


Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba akipokea msaada wa madawati kutoka kwa mwasisi wa Taasisi ya Kijana Kwanza Apaikunda Naburi, katika tukio lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya Reginald Mengi.
Taasisi ya Kijana Kwanza ya Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro imetoa msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 14 kwa shule ya sekondari ya Reginald Mengi. 

Msaada huo umepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba katika tukio lililofanyika shuleni hapo mchana wa leo. 

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Reginald Mengi baada ya kupokea madawati 100 waliyoyakalia kutoka Taasisi ya Kijana Kwanza.

Wanafunzi ya Shule ya Sekondari ya Reginald Mengi, mjini Moshi wakifuatilia jambo.

Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Moshi Angelina akisisitiza jambo katika tukio la kupokea madawati  100 kutoka kwa Taasisi ya Kijana Kwanza, hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Reginald Mengi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Reginald Mengi Mkude Missoti akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba akifurahia jambo wakati wa kupokea madawati kutoka kwa Taasisi ya Kijana Kwanza, hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Reginald Mengi.




STORY & PHOTO BY: Jabir Johnson
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com 
DATE: March 2, 2020

Wito umetolewa kwa wanafunzi wa sekondari mjini Moshi kuacha mara moja vitendo vya utovu wa nidhamu kwani kwa kuendelea kufanya kutaathiri mfumo mzima wa kufundisha na kujifunza.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 100 kwa shule ya Sekondari ya Reginald Mengi yaliyotolewa na Taasisi ya Kijana Kwanza ya mjini Moshi, Mkuu wa Wilaya hiyo Kippi Warioba alisema tabia za mbaya za wanafunzi ndio sababu kubwa ya kuzorota kwa maendeleo ya mwanafunzi mwenyewe na jamii kwa ujumla.

“Mtoto wa mjini anatakiwa kuwa mjanja katika kuitafuta elimu na kujiongezea maarifa, ujanja sio kuvuka barabara na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu, hatutakiwi kwenda namna hiyo.” alisema Mkuu wa Wilaya hiyo.

Aidha Warioba aliwataka wanafunzi hao kujiepusha na kuzoeana na watu wasiowafahamu, madereva bodaboda, kupewa lifti ili kujikita katika kujiongezea maarifa hali ambayo itawaleta wadau zaidi wa elimu kujitolea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza.

Warioba alisema kupata msaada ni jambo jema kwa wanafunzi hao na maendeleo kwa jamiii na kwamba wayatumie vizuri, wayatunze kwa kujifunza na kuinua viwango vyao vya elimu.   

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Kijana Kwanza Sadat Ndibalema alisema wameendelea kutoa msaada kwa shule hiyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunza.

“Madawati haya yana thamani ya shilingi milioni 14 tumeyatoa katika shule hii (Reginald Mengi) ili kuunga mkono juhudi za wadau wa elimu kuboresha mazingira ya kujifunzia,” alisema.

Shule ya sekondari Reginald Mengi ilikuwa ndio shule yenye nidhamu mbovu lakini wadau wa elimu wamepambana hadi kuifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule bora katika manispaa ya Moshi na sisi kwa kuona hivyo tumeamua kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kutoa madawati haya,” aliongeza.

Kwa upande wake Mwasisi wa Taasisi ya Kijana Kwanza Apaikunda Naburi alisema kwa sasa taasisi yake inawalea vijana 23 ambao walikuwa katika mazingira magumu kufikia matarajio yao kwa kuwapeleka shuleni na wanasoma katika shule za sekondari zilizopo mjini Moshi.

0 Comments:

Post a Comment