Kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) |
Leo ni maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini.
Kauli mbiu ya maadhimisho mwaka huu; "CCM tumeahidi, tumetekeleza na tunaahidi tena kuchapa kazi kwa juhudi, ubunifu na maarifa zaidi hapa kazi tu."
Mapendekezo ya kuundwa kwa Chama Cha Mapinduzi yalitolewa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Katika kikao cha pamoja cha NEC ya TANU na NEC ya Chama Cha ASP cha Zanzibar, kilichofanyika Dar es Salaam, Septemba 5, 1975, ili kuimarisha zaidi Muungano.
Rais wa Zanzibar wa wakati huo Alhaji Abdul Jumbe alikubali kimsingi wazo hilo, lakini akataka ASP kipewe muda kufikiria zaidi. Mwaka mmoja baadaye, Oktoba 1976, maridhiano yakafikiwa ya kuunda Chama kipya Chama cha Mapinduzi' (CCM), kilichozinduliwa Februari 5, 1977, tarehe na mwezi sawa na ilipozaliwa ASP miaka 20 nyuma, mwaka 1957.
Licha ya Wazanzibari kushinikiza tarehe na mwezi wa kuzaliwa chama chao cha ASP iwe ndio tarehe na mwezi wa kuzaliwa CCM, yaani Februari 5, walishinikiza pia na kufanikiwa kubakiza neno ‘Mapinduzi' yaliyoleta uhuru wao Januari 12, 1964, liwe sehemu ya jina la chama kipya. Kwa maana ya Chama cha Mapinduzi bila kuwa na tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza.
Hizo ndizo zilikuwa karata mbili pekee kwa Wazanzibari kukubali kuunda Chama kipya, chama ambacho kilipewa ukuu wa kikatiba wa kushika hatamu zote za uongozi wa nchi.
Hivyo basi historia inaonyesha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa Februari 5, 1977 baada ya kuvunjwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shirazi Party (ASP).
Chama cha ASP kwa upande wa Zanzibar kilitokana na muungano wa African Association (AA) na Shirazi Association (SA), ikiwa ni kuunganisha nguvu za wanyonge katika mapambano ya kuuondoa usultani na utawala wa kikoloni wa Kiingereza.
Kwa upande wa Tanzania Bara, TANU ilizaliwa kutokana na kujibadilisha kwa Tanganyika African Association (TAA) kutoka jumuiya ya kutetea maslahi ya kijamii na kuwa chama cha siasa.
Uhuru wa Tanganyika wa Desemba 9 mwaka 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, kulifanya TANU na ASP vikamilishe kazi ya ukombozi wa nchi hizi mbili kutoka katika makucha ya ukoloni mkongwe na usultani.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kupewa dhamana ya kuunda serikali na kushika dola tangu 1977 chini ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja hadi sasa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kufuatia mageuzi yaliyoidhinishwa na marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1992.
Aidha, tangu kuanzishwa kwa CCM, Februari 5 ya kila mwaka, chama hicho kimekuwa kikiadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwake, ambapo jana kilitimiza miaka 42 tangu kianzishwe mwaka 1977.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) John Pombe Magufuli |
0 Comments:
Post a Comment