Mkazi wa kijiji cha Mandaka Mnono wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro amekutwa ameuawa kikatili kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na kutupwa shambani.
Tukio hilo limetokea hivi karibuni katika kitongoji cha Saning'o wilayani Moshi mkoani hapa marehemu aliyefahamika kwa jina la Thobias Laurent Makoma anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 61 alifanyiwa unyama huo.
Chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa ni kugombania mwanamke baina ya marehemu na mkazi mmoja kijijini hapo aliyefahamika kwa jina la Ngosha anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 55 ambaye hujishughulisha na kazi za vibarua.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema ndugu, jamaa na marafiki walishtuka mnamo Februari 4 mwaka huu kumkosa katika maeneo ambayo walizoea kumuona kwani marehemu alikuwa alikuwa akishughulisha na shughuli za ukulima.
"Hatukumuona siku tatu kijiweni tunapokutana ndipo tulipoenda nyumbani kwake na kukuta milango imefungwa, tukapiga ukunga (filimbi ya wito) kuanza kumtafuta ndipo jana (Februari 4) tukaukuta mwili wake ukiwa shambani," alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Steven Michael.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa kijiji cha Mandaka Mnono walisema muuaji alikuwa ameanza kujenga mahusiano na mwanamke mmoja (jina limehifadhiwa) ambaye kazi yake ilikuwa ni mama lishe na ukulima.
"Kwa kweli hawa wawili tunahisi kuwa ni kugombania mwanamke mpika chai na chapati ndio kulikofanya mmojawapo kupoteza maisha, Ngosha alimlia timing marehemu akiwa shambani kwake na kumuua kikatili licha kwamba hakukuwa na dalili za wazi za ugomvi wao," aliongeza shuhuda mmoja.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Charles Morris Ngoma amesema baada ya kuukuta mwili huo katika shamba lake lililopo katika kitongoji cha Saning'o waliamua kumtafuta muuaji ambaye walifanikiwa kumpata.
Pia muuaji ambaye anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro inadaiwa alipotekeleza mauaji hayo alichukua funguo za nyumba ya marehemu na kwenda kubeba baadhi ya vyombo vya marehemu na kwenda kuviuza.
Marehemu amepoteza maisha akiwa ameacha watoto saba, wawili wa kike na watano wa kiume ambao kila mmoja anaishi kwake, hivyo hadi mauti yanamkuta marehemu alikuwa akiishi peke yake.
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kwamba upelelezi zaidi unaendelea ambapo jioni ya Februari 4 mwaka huu walitoa ruhusa ya kuuzika mwili wa marehemu kutokana na kwamba ulianza kuharibika.
Tukio la kuuhifadhi mwili wa marehemu katika nyumba ya milele lilifanyika Februari 5 mwaka huu katika makaburi ya kijiji cha Mandaka Mnono.
STORY BY: Jabir Johnson, Moshi..................................Februari 7, 2020
0 Comments:
Post a Comment