Miili 20 ya watu waliofariki baada ya kukanyagana mjini Moshi mkoani wa Kilimanjaro inatarajiwa kuagwa katika tukio la kitaifa kwenye uwanja wa Majengo kulikotokea tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa imesema miili 16 imeshatambuliwa na ndugu zao hukuu minne ikiwa bado haijatambuliwa.
Tukio hilo linatarajiwa kuanza majira ya saa nne asubuhi ambapo miili ya marehemu hao itatolewa mochwari na kupelekwa katika uwanja huo kisha ndugu watakabidhiwa kuendelea na taratibu zao huku ile ambayo haijatambulika itarudishwa mochwari hadi itakapotambulika na kama bado serikali itaihifadhi katika nyumba ya milele.
Miili hiyo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi Maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mawezi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Watu hao walifariki dunia baada ya kukanyagwa na wenzao wakati wakitoka katika lango moja waliloelekezwa kupita ili kukanyaga mafuta ya upako katika huduma ya Inuka Uangaze inayoongoza na Mtume na Nabii Boniface Mwamposa maarufu Bulldozer Februari 1, 2020.
Mwamposa alilazimika leo Jumapili kuahirisha ibada tofauti na ilivyozoeleka na kujisalimisha katika vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kuitikia wito wa Polisi mkoani Kilimanjaro, kulikotokea vifo vya waumini wake.
Taarifa zinasema utaratibu katika ibada zake huko Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam humaliza saa saba za mchana lakini leo Februari 2, 2020 amemaliza ibada saa 4:30 asubuhi ili kuitikia wito huo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli (JPM) hapo jana alituma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliopoteza maisha wakati wakitoka katika Ibada hiyo.
JPM alieleza kusikitishwa na idadi kubwa ya vifo vya Watanzania waliopoteza maisha katika matukio hayo na amewaombea marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao.
Inakadiriwa kuwa watu waliohudhuria ibada hiyo ya Utakaso walikuwa zaidi ya 4,500 na sio mara ya kwanza kwa Mwamposa kufanya ibada kama hizo katika uwanja huo huku ikitajwa kuwa amekuwa na utaratibu huo kwa muda sasa katika Kanisa lake hilo la Inuka na Uangaze.
STORY BY: Jabir Johnson, Moshi..............................Februari 2, 2020
0 Comments:
Post a Comment