Februari 14, 2004 ilikuwa Siku ya Wapendanao maarufu kama Valentine Day.
Siku hii timu ya taifa la Tunisia ya mpira wa miguu iliwapa zawadi wapenzi na mashabiki wake kwa kutwaa taji la Mataifa ya Afrika (AFCON) likiwa ni taji lao la kwanza kuwahi kulitwaa baada ya kuizabua Morocco kwa mabao 2-1.
Mwewe wa Carthage walifanikiwa kutwaa taji hilo kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa hilo ambao ni mkubwa nchini humo wa Novemba 7 katika jiji la Rades.
Mwaka 2004 ilikuwa ni mara ya tatu kwa taifa hilo kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya soka ambapo Tunisia iliwahi kuwa wenyeji mwaka 1965 na kusalia kutwaa nafasi ya pili wakishindwa mbele ya Ghana na mnamo mwaka 1994 Mwewe hao wa Carthage waliondolewa kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Tunisia ilikuwa imara mno katika michuano ya mwaka 2004 ikianza kwenye hatu ya makundi dhidi ya Guinea , Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika hatua ya makundi Tunisia ilishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya DRC na iliweka rekodi ya kushinda mchezo kwa zaidi ya bao moja.
Katika hatua ya mtoano Tunisia ilifanikiwa kuizabua Senegal kwa bao 1-0 katika robo fainali kabla ya kupata changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya Nigeria katika nusu fainali.
Dakika 90 zilimalizika kwa sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa nyongeza mshambuliaji wa Nigeria Osaze Odemwingie alikosa na kuipa Tunisia kwa mikwaju 5-4 na kusonga mbele katika fainali.
Katika mchezo wa fainali dhidi ya Morocco dakika ya tano ya mchezo Tunisia ilipata uongozi kutoka kwa mshambuliaji wao Francileudo dos Santos. Morocco walisawazisha katika dakika ya 38 ya mchezo kupitia kwa kiungo wake Youssef Mokhtari kabla ya mshambuliaji wa Tunisia Ziad Jaziri kufumania nyavu katika dakika ya 52 uliwapa taji hilo.
Wakati Dos Santos anafunga bao hilo lilikuwa la nne katika mashindano hayo akiwania kiatu cha dhahabu. Mpaka Dos Santos ambaye alizaliwa Brazil anaongoza kwa ufungaji wa mabao katika timu ya taifa ya Tunisia akiwa ametupia mabao 22 katika mechi 40 alizocheza.
Bao lake lake la kwanza alilifunga Januari 17, 2004. Anayemfuata Adel Sellimi aliyefunga mabao 19, bao lake la kwanza alifunga Oktoba 11, 1992 hadi kustaafu kwake Januari 23, 2000.
Baada ya kuchukua taji hilo Tunisia imekuwa ikipambana kutaka kurudi katika rekodi ya mwaka 2004 bila mafanikio.
0 Comments:
Post a Comment