Thursday, February 13, 2020

Unamkumbuka Pierluigi Collina?

Februari 13, 1960 alizaliwa mwamuzi maarufu raia wa Italia Pierluigi Collina. Collina alizaliwa mjini Bologna. 

Mwamuzi huyo anafahamika sana na wapenzi na mashabiki wa soka ulimwenguni kutokana na mwonekano wake usiokuwa na shaka na maamuzi yake kwenye soka akipendelea kunyoa upara na macho yake makubwa. 

Collina aliwahi kutwaa mara sita tuzo za Mwamuzi Bora wa Dunia wa Mwaka. Aliamua katika mashindano makubwa ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na Fainali za Kombe la Dunia. 

Medani ya uamuzi katika soka alianza mnamo mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 17 tu na kwa haraka alikua na kung'ara hivyo kuingia katika Serie C1 na Serie C2 mnamo mwaka 1988. Miaka mitatu baadaye alifanikiwa kupanda daraja la kuwa mwamuzi wa Seria A na Serie B. 

Mnamo mwaka 1996 kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya uamuzi wa soka alichezesha mchezo wa kimataifa wa fainali baina ya Argentina na Nigeria katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Atalanta nchini Marekani.

Mnamo mwaka 1999 alikuwa mwamuzi wa fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baina ya Bayern Munich na Manchester United uliochezwa katika dimba la Camp Nou, Hispania.

Ilipofika mwaka 2002 alipanda viwango pale alipochezesha fainali ya Kombe la Dunia baina Brazil na Ujerumani mchezo ulichezwa katika Uga wa Kimataifa wa Yokohama nchini Japan.

Kutoka mwaka 1998 hadi 2003 Collina alitwaa tuzo sita za mwamuzi bora wa mwaka. Enzi zake akiwa dimbani alionyesha umahiri mkubwa na taaluma kubwa.

Mnamo mwaka 2006 wakati Italia ilipokumbwa na kashfa ya upangaji wa matokeo Mkurugenzi wa klabu ya Juventus Luciano Moggi ambaye alikuwa miongoni mwa wanaohusika na mipango ya siri katika kashfa hiyo aliielezea polisi ya Italia kuwa Collina hakuwahi kujihusisha na kupanga matokeo yoyote katika mchezo wa soka.

 Collina alistaafu medani ya uamuzi mnamo mwaka 2005 lakini bado anaendelea kujihusisha na masuala ya michezo, tangu mwaka 2010 amekuwa katika Shirikisho la Soka la Ukraine kama Mkuu wa Waamuzi wa taifa hilo.

0 Comments:

Post a Comment