Saturday, February 15, 2020

RC Kilimanjaro aagiza Mkurugenzi Lubuva kutolipwa mshahara

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ameagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zefrin Lubuva kutolipwa mshahara wa Februari mpaka atakapojirekebisha.

Sakata hilo limetokea February 14, katika kikao maalumu cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa cha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021.

Mkurugenzi huyo alishindwa kujibu kwanini Halmashauri hiyo imeshindwa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Walemavu.

Kila Halmashauri hutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwapa mikopo isiyo na riba Vijana, Walemavu na Wanawake.

Hivi karibuni Madiwani wa halmashauri hiyo waliazimia kutofanya kazi na mkurugenzi huyo na badala yake, madiwani hao wakiongozwa na mwenyekiti wao,Theresia Msuya wamemuomba Rais John Magufuli kuwapelekea mkurugenzi mwingine wakidai Lubuva hana uwezo.

Uamuzi huo ulichukuliwa katika kikao cha kawaida cha madiwani, wanamtuhumu Lubuva kukaidi maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Katika kikao hicho, ilielezwa kuwa Majaliwa aliagiza barua zote za onyo alizoziandika Lubuva kwa watumishi zifutwe na wakuu wa idara aliowahamisha warejeshwe.

Hata hivyo, katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na mkuu wa wilaya ya Mwanga, Thomas Apson, madiwani walidai maagizo hayo na mengine hayakutekelezwa.

Akichangia diwani wa ya Kigonigoni, Jeremiah Shayo alidai muda mrefu kumekuwa na msuguano kati ya Lubuva na kamati ya fedha kuhusu ukusanyaji mapato.

“Tumechaguliwa na wananchi kusimamia halmashauri hii hatuko tayari kufanya kazi na huyu mkurugenzi na Rais asikie kilio chetu ambadilishe atuletee mwingine,” alieleza Shayo.

0 Comments:

Post a Comment