Februari 1, 2012 ilikuwa siku mbaya katika soka la nchini Misri baada ya watazamaji 79 kufariki dunia na zaidi ya 1,000 kujeruhiwa baada ya vurugu kuibuka kwenye mchezo wa ligi kuu nchini humo.
Mchezo wa Ligi Kuu nchini Misri ulikuwa kati ya Al Ahly na Al Masry katika dimba la Port Said zamani ukifahamika kwa jina la Al Masry Club Stadium. Tangu mwanzoni mwa mchezo huo ilonekana kuwa usingemalizika salama kwani dakika 30 zilipotea kabla ya mchezo kuanza.
Wenyeji wa mchezo huo walishinda kwa mabao 3-1, kila bao lilipokuwa likifungwa na wenyeji wa mchezo huo mashabiki walivamia uwanja.
Baada ya mchezo kumalizika, baadhi ya wapenzi na mashabiki wa Al Masry walivamia uwanja na kuwavamia wachezaji na mashabiki wa Al Ahly wakitumia visu, fimbo na mawe.
Jumla ya watu 79 waliuawa kutokana na kuchomwa na visu, kupigwa na wengine kukanyagana wakati wa purukushani hilo huku maelfu ya wengi wakisalia kuwa majeruhi.
Baada ya tukio hilo watu wengi walikaririwa wakisema siasa ndio chanzo cha vurugu hizo huku wakivinyoshea kidole cha lawama vyombo vya ulinzi na usalama nchini humo kuwa walionyesha nia ya kuwapiga wapenzi na mashabiki wa Al Ahly ambao walionekana kuunga mkono mapinduzi ya Misri mwaka mmoja kabla yaliyomweka madarakani rais wa zamani wa taifa hilo Mohamed Mursi.
Mamlaka nchini Misri ziliwakamata watu 73 ambapo 21 katii hayo walihukumiwa kunyongwa Januari 2013 hali ambayo iliibua vurugu ambazo zilikuwa kubwa kuliko za awali.
Baada ya mapingamizi idadi ya watu wa kunyongwa ilipungua na kusalia watu 10. Wengi wa waliopandishwa kizimbani walihukumiwa kwenda jela kati ya miaka 5 hadi 15. Wengine waliachiwa huru.
Bunge la nchi hiyo liliita kikao cha dharura kujadili hali hiyo Februari 2, 2012. Spika wa Bunge Saad El-Katatni wa Udugu wa Kiislamu alihoji vyombo vya ulinzi na usalama namna vilivyojaribu kuzuia vurugu hizo tangu mwanzo.
Mechi zilizokuwa zichezwa ziliahirishwa ikiwamo ya Zamalek na Ismailia. Machi 10, 2012 chama cha soka cha Misri kilitangaza kuwa mechi zilizosalia kwa msimu huo hazitachezwa.
Matokeo ya vurugu hizo ni kwamba serikali ya Misri iliifungia ligi kuu nchini humo kwa miaka miwili hali iliyoathiri pakubwa timu ya taifa hilo katika mashindano ya kimataifa.
Rais wa shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA) wakati huo Sepp Blatter alisema tukio hilo ni la kuhuzunisha huku akionyesha huruma kwa familia zilizopotelewa na ndugu zao katika vurugu hizo huku akitoa msisitizo kuwa haipaswi tukio kama hilo kutokea tena.
0 Comments:
Post a Comment