Monday, February 3, 2020

Simanzi yatanda kuagwa kwa miili 20 waliokufa kwa Mwamposa

Simanzi imetanda katika tukio la kuagwa kwa miili ya watu waliofariki wakati wakihudhuria ibada katika Kanisa la Inuka na Uangaze Februari Mosi mwaka huu linaloongozwa na Mtume na Nabii Boniface Mwamposa maarufu Bulldozer.

Tukio hilo la kuagwa kwa miili ya marehemu hao limefanyika katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi, Kilimanjaro Februari 3 mwaka huu na kuhudhuriwa na watu kutoka viunga mbalimbali mkoani humo.

Miili ya watu 20 waliopoteza maisha wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto iliwasili katika viwanja hivyo saa 5: 56 asubuhi ikiwa katika magari ya Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro aina  ya Ashok Leyland PT 4062 na PT 4374.

Baada ya kufika viwanjani hapo ilipokelewa kwa hisia za huzuni na majonzi huku wengine wakibubujikwa na machozi wakishindwa kuamini kama ndugu, jamaa na marafiki wao wakiwa ndani ya majeneza tayari kufanyiwa sala ya pamoja kisha kukabidhiwa kwa ajili ya utaratibu wa familia.

KAMANDA WA POLISI ATOA TAARIFA YA TUKIO LILIVYOKUWA
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) mkoa wa Kilimanjaro Said Hamduni alisema Mwamposa aliomba kibali cha siku tatu cha mkutano wake katika uwanja wa Majengo kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 jioni.

Aidha ACP Hamduni alisema mpaka sasa Jeshi la Polisi limewakamata watu saba kwa mahojiano zaidi akiwamo Mtume na Nabii  wa huduma hiyo ya Inuka na Uangaze Boniface Mwamposa kuhusiana na tukio hilo na kwamba sheria itafuata mkondo wake.

Katika tukio hilo watoto waliopoteza maisha ni watano na mwanaume mmoja huku wanawake wakiwa ni 14.
Nabii na Mtume Boniface Mwamposa wa Huduma ya Inuka na Uangaze.

0 Comments:

Post a Comment