Wednesday, February 26, 2020

Unaikumbuka siku ya kwanza ya Roberto Carlos kuitumikia Brazil?


Februari 26, 1992 mlinzi wa kushoto wa Brazil Roberto Carlos aliiitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa kwenye mchezo wa kirafiki ambao Seleccao walishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Marekani.

Baada ya hapo alicheza jumla ya mechi 125 akiwa na Seleccao na kushika nafasi ya pili kwa kuwa mchezaji aliyehudumu na miamba hiyo kwa kucheza mechi nyingi.

Aliitwa katika kikosi hicho akiwa na umri wa miaka 18 wakati huo ndiyo kwanza alikuwa ameanza safari yake ya soka katika medani ya kimataifa akiwa na klabu ya Serie B ya União São João miaka miwili kabla.

Kuitwa kwa nyota huyo kuliwastaajabisha wengi, lakini Kocha wa wakati huo Carlos Alberto Parreira ambaye alikuwa ametoka kuchukua wadhifa wa kuiongoza miamba hiyo alikuwa akitaka damu mpya ya vijana katika kikosi.

Hatua hiyo aliifikia kutokana na matokeo mabaya kwenye Kombe la Dunia mnamo mwaka 1990.
Mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Marekani ulichezwa katika mji wa nyumbani kwa nyota huyo wa Fortaleza.

Hakika Roberto Carlos alionyesha kuwa sio wa mchezo mchezo akiisaidia Brazil kutoruhusu wavu wake kutikiswa dhidi ya Wamarekani hao.

Zaidi sana mlinzi mwenzake Antonio Carlos alitupia bao la tatu akipokea pasi murua ya kiungo Rai na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0.

Hata hivyo Carlos alikosa fainali za Kombe la Dunia mnamo mwaka 1994 na alikuwa miongoni mwa waliochaguliwa katika kikosi bora cha Kombe la Dunia mwaka 1998 na 2002. 

Mnamo mwaka 2002 akiwa na Brazil alifanikiwa kutwaa taji hilo.

Mchezo wake wa mwisho katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil ilikuwa ni Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani, ambako walitolewa katika robo fainali na Ufaransa.



0 Comments:

Post a Comment