Mwanafunzi Juliana Julius (14) anayesoma darasa la sita katika shule ya Msingi Bunge iliyopo Kata ya Mabilioni, wilayani Same mkoani Kilimanjaro, ameuawa na Kiboko wakati alipokwenda kuoga katika mto Pangani.
Akizungumza na wakazi wa kitongoji cha Bunge kata ya Mabilioni, wakati wa msako wa kumtafuta mwanafunzi huyo Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule, amelazimika kupiga marufuku wananchi kwenda kuoga na kuchota maji kwenye mto Pangani kutokana na matukio ya watu mbalimbali kuuawa na viboko.
Senyamule alisema kutokana na matukio ya watu kuuawa na viboko kwenye mto Pangani hadi sasa watu wanne wameuawa hivyo amelazimika kufunga matumizi ya kibinadamu katika mto huo ili kuokoa maisha yao.
“Katika kipindi cha miaka mitatu watu wanne wameripotiwa kuwa wameshakufa, hivyo kutokana na matukio haya serikali inalazimika kufunga shughuli zozote zinazofanyika kwenye mto huu ikiwemo kuoga, kufua ama kuvua ,”alisema.
Aidha DC Senyamule alisema kuwa baada ya tukio hilo msako mkali ulianza wa kumtafuta mwanafunzi huyo ili kuokoa maisha yake, lakini zoezi hilo halikufanikiwa, mpaka siku iliyofuata ambapo mabaki ya mwili huo yalipopatikana kwenye kijiji jirani cha Kidungai kilichopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Alifafanua kuwa mwili huo ulipatiikana kwa ushirikiano wa Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, askari wa wanyamapori na wananchi huku akitoa maagizo kwa idara ya maliasili kuhakikisha kwamba wanamuua mnyama huyo ili asiendelee kuleta madhara kwa binadamu.
Matukio ya watu kuuawa na mamba na Kiboko katika mto Pangani yameendelea kushika kasi huku uongozi wa wilaya ya Same wakiumiza vichwa kutafuta namna ya kuwadhibiti wanyama hao.
STORY BY: Kija Elias, Same......Februari 14, 2020
0 Comments:
Post a Comment