Wednesday, February 26, 2020

Polisi Tanzania 1-1 Yanga SC: Walichinja Paka wakaambulia sare Ushirika




NA JABIR JOHNSON
Februari 18, 2020 kulichezwa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara katika dimba la Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro. 

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1 baina ya wenyeji Polisi Tanzania na Yanga SC. Mabao ya Tariq Seif wa Yanga na Sixtus Sabilo wa Polisi Tanzania yalitosha kutoa sare hiyo. 

Miongoni mwa michezo iliyokuwa na msisimko mkali ulikuwa ni huo kutokana na historia ya timu kutoka Dar es Salaam kwa miaka mingi zinapotua katika mji wa Moshi. 

Ikiwa imepita takribani miongo mitatu ya kutoziona timu za ligi kuu msimu wa 2019/2020 umeweka historia kwa wakazi wa Kilimanjaro na vitongoji vyake. 

Itakumbukwa mchezo wa kirafiki Yanga ilizabuliwa mabao 2-0 na Polisi Tanzania; baada ya kutua katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Polisi Tanzania ililazimisha sare ya 3-3 na mzunguko wa pili tena ililazimisha sare ya 1-1. 

Hata hivyo kwenye mchezo huo uliochezwa Moshi umeacha maswali mengi kutokana na mambo kadhaa ambayo ni vema ukayafahamu kuwa yalikuwepo kwenye mchezo huo.

1. Kuchinjwa kwa Paka
Macho yalishuhudia paka aliyebebwa na mojawapo wa mashabiki siku moja kabla ya mchezo huo na kushangaza zaidi ni kwamba katika ngazi za kupandia vyumba vya kubadilishia wachezaji wa Yanga vilivyoko upande wa goli la kaskazini ya Uwanja; kulikuwa na viashara vya damu ambayo inasadikika kuwa ya paka. 

Hili lilijihidhirisha siku ya mechi kwani Yanga hawakutaka kuingia katika vyumba vya kubadilishia na walisalia kukaa nje kwenye viti vyeupe vilivyoandaliwa kutokana na kuwa na wasiwasi mpaka pale walipojiridhisha kuwa kuna usalama. 

Maswali ni haya Paka yule siku moja kabla ya mchezo ni wa nani? alitoka wapi kwani ni nadra kuona Paka wakisafirishwa kama kuku na mbwa?; Kama alichinjwa, alichinjwa kwa sababu gani? na kama ni ushirikina ni mganga gani aliyehusika katika hilo na kwa watu wapi? Je ni timu au mashabiki wa timu? 

Haya ni baadhi ya maswali ambayo ni magumu mno kuyajibu. Lakini ukweli Paka alichinjwa.


2. Kijana na Bango la Bangi atolewa
Siku ya mchezo kama kawaida katika Ligi Kuu utani wa jadi baina ya Simba na Yanga kote nchini ni hali ya kawaida; kuwaona mashabiki wa timu hizo wakitambiana kwa tambo mbalimbali hata kama timu yake haichezi siku husika. 

Kijana mmoja aliyekuwa katika jukwaa la Polisi Tanzania ambaye jina lake halikupatikana mara moja aliandika bango lililokuwa na maneno 'Bangi iruhusiwe..." huku akiwa ametengeneza kipande cha gazeti kilicho na mfano wa msokoto. 

Kijana huyo alikuwa akitambiana na mwenzake wa jukwaa la Yanga.

Lakini cha kustaajabisha kijana huyo alibebwa mzegamzega kwenye gari la jeshi la Polisi na kwenda kuhojiwa eti kwa kuhamasisha watu kuvuta dawa za kulevya. 

Hivi linaingia akilini kwenye michezo suala hilo. Haijulikani hadi sasa nini kinaendelea kwa kijana huyo aliyekatishwa kutazama mchezo huo.

3. Kiongozi wa soka kuiba tiketi
Suala la wizi wa tiketi limekuwa likipigiwa kelele mno na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), katika mchezo huo kiongozi mmoja wa soka (jina tumelihifadhi kutovuruga uchunguzi) aliyekuwa katika geti akiruhusu watu kupita alipokuwa akipokea tiketi badala ya kuchana alikuwa anazificha kisha kwenda kuziuza kwa mara ya pili. 

Hata hivyo mamlaka zilizokuwepo zilifanya kazi nzuri na kubaini ukiukwaji kanuni za soka na sheria kwa ujumla na kumtia nguvu kwa ajili kujibu tuhuma hizo.

4. Ulinzi wa Farasi na Mbwa tafrani
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA ) limekuwa likijitahidi kusisitiza kuhusu uwepo wa vyombo vya ulinzi na usalama katika viwanja vya michezo duniani. 

Pia FIFA pamoja na vyombo vyake limekuwa likiweka taratibu ya namna vyombo hivyo vinatakiwa kusimamia mchezo wa soka. 

Cha kustaajabisha ni kwamba askari wa Jeshi la Polisi walikuwa wengi katika uwanja wa Ushirika kushuhudia mchezo huo huku wakiwa katika mavazi ya kazi. 

Kama haitoshi waliingia na Farasi na mbwa wa Kijeshi pia mabomu ya machozi.

Kitendo hicho kilisikitisha sana kwani kufanya hivyo kungeweza kuleta maafa makubwa zaidi ya Mwamposa. 

Ukweli ni kwamba askari wengi walitumia kigezo cha mavazi yao na kazi yao kwa ujumla kupata nafasi ya kutazama mchezo huo. 

Halafu wenye farasi na wenyewe kwa kutaka sifa wakapita nazo pembeni ya uwanja wa kuchezea mpira kwa kasi. 

Kisaikolojia wachezaji na mashabiki wa soka walikuwa katika wakati mgumu kutambua kuwa ile ni burudani au ni ujio wa kiongozi wa kisiasa katika kufanya uzinduzi wa jambo fulani la kitaifa au kimataifa.

Sheria za soka katika ulinzi zimekaaje? Askari Polisi wanazifahamu? au ndio kiburi kutokana na idadi kubwa ya watanzania wapenda soka kutojua haki na wajibu wao?

5. Watu kupanda miti na kuta za Uwanja
Wapenzi na mashabiki wa soka walionekana kwenye miti inayozunguka Uwanja huo wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi na wengine walipanda kabisa katika kuta za uwanja huo kushuhudia mchezo huo. 

Swali la kujiuliza, hivi ingetokea wangeanguka na kupoteza maisha tungeuambia nini ulimwengu kuhusu maafa hayo ya kizembe? 

Askari Polisi walio wengi walikuwa ndani wanatazama  mchezo huo na farasi na mbwa zao. 
Awali walijaribu kuwatoa lakini kwasababu ya kuipenda zaidi mechi hiyo badala ya kudhibiti mihemko yao wakiwa kazini; wale mashabiki walirudi tena kwenye matawi ya miti kama Tarzan.
Charles Boniface Mkwasa

Malale Hamsini

6. Wanahabari Kilimanjaro njiapanda
Hapa ilikuwa changamoto hususani kwa wanahabari wa mkoa wa Kilimanjaro. 

Kiukweli ni kwamba waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro walio wengi sio waandishi wa habari za michezo na burudani walio wengi wemejikita katika masuala mengine. 

Sasa usumbufu uliojitokeza hapo ni kwa wale wasiojua kwa kina mchezo wa soka kufikiri kuwa wataingia tu kama wanavyoingia katika maeneo mengine hususani wale wenye mapenzi motomoto na timu hizi kubwa Simba na Yanga. 

Lakini kama haitoshi wakati wa kuchukua habari zenyewe hawajui nani ni nani; kwa kiasi fulani ilisikitisha mno. 

Wadau wa soka mkoani Kilimanjaro wamekuwa na tabia ya kulaumu kuwa kwanini habari nyingi za michezo mkoani Kilimanjaro sio za viwango lakini ukweli ndio huo kuwa wengi sio wabobezi katika michezo na burudani hususani soka. 

Katika hili ningeomba mamlaka husika ziwe zinafika mikoani kutoa semina kwa waandishi wa habari kuhusu michezo yao hususani soka na isiwe Dar es Salaam pekee ili kuondoa usumbufu na hii itasaidia kuinua soka katika mkoa na taifa kwa ujumla.

Imetayarishwa na Jabir Johnson kwa maoni na ushauri +255 768 096 793 au baruapepe: jabirjohnson2020@gmail.com





0 Comments:

Post a Comment