Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya mkoa na ile ya Wilaya, wakiwa wanakunywa maji ya mtiririko kwenye mradi wa maji Njoro. |
Kamati ya Siasa ya
Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, imesema kuwa Serikali ya Awamu ya
Tano, imefanikiwa kuboresha maisha ya wananchi wake, kupitia miradi mbalimbali.
Hayo yamesemwa Jana na
Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Jonathan Mabihya, wakati wa ziara ya kukagua
na kutembelea mradi wa ujenzi wa maji ya mtiririko Njoro, Wilaya ya Rombo
mkoani humo.
Alisema dhamira ya
viongozi waliopo madarakani chini ya Rais Dkt. Magufuli ni kuhakikisha
wanatekeleza kwa ukamilifu Ilani ya CCM ya Mwaka 2015/2020.
"Serikali iliyopo
chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt.
Magufuli, imefanya kazi kubwa kwenye utelekezaji wa Ilani ya CCM, hivi sasa
inaendelea kujenga miundombinu ya barabara, reli, maji na vituo vya
afya,"alisema Mabihya.
Aidha Kamati hiyo ya
Siasa ya mkoa na ile ya Wilaya ya Rombo, pia walitembelea ujenzi wa vyumba
viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Nduweni na ujenzi wa bweni la
wasichana katika shule ya sekondari Motamburu.
Mabihya alifafanua
kuwa "Lengo la ziara hii ni kukagua utelekezaji wa Ilani ya CCM
katika kipindi cha miaka mitano tangu wananchi walipoipa CCM ridhaa ya
kuongoza nchi mwaka 2015 na kumchagua Rais Dkt. Magufuli ili aweze
kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano,".
Aliongeza kuwa
"Unapopewa uongozi, lazima ujitathmini , hivyo Kamati ya Siasa ya mkoa na
ile ya Wilaya tupo hapa kwa ajili ya kutathmini yale tuliyoyaahidi kwa
wananchi katika kipindi cha miaka mitano," alisema Mabihya.
Alisema kwenye mafanikio
hapakosi changamoto, hivyo katika ziara hii, Kamati ya Siasa ya mkoa
imeona ni vyema kuipitia miradi iliyokwisha kutekelezwa na endapo kuna
changamoto zilizojitokeza iweze kuzifanyia kazi.
Akisoma taarifa ya
mradi wa maji Njoro II Meneja mradi wa Kampuni ya Kiliwater Prosper Kessy,
alisema mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha Sh bilioni 1.7
"Mradi huu hadi
kukamilika utanufaisha wananchi 24,684, na hivyo kupunguza changamoto ya maji
kwa asilimia 13," alisema.
Naye Mkuu wa shule ya
sekondari Nduweni Raphael Kital, alisema shule ina idadi ya wanafunzi 568
ambapo wavulana ni 269 na wasichana ni 299.
"Shule ina vyumba
vya madarasa tisa, kwa sasa shule ina kabiliwa na upungufu wa madarasa matano,
kutokana na changamoto hiyo uongozi wa Serikali ya kijiji na kata umefanya
jitihada za dhati za kupunguza changamoto hiyo kwa kununua eneo jipya kwa ajili
ya mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa viwili,"alisema.
Awali Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Rombo Godwin Chacha, alisema halmashauri
hiyo itachangia mabati ili kuweza kuwaunga mkono wananchi waliojitolea
nguvu kazi zao za kujenda madarasa hayo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rombo Anthony Tesha, alichangia mifuko ya saruji
10 katika kuwaunga mkono huku CCM mkoa nao wakichangia mifuko ya saruji
30.
Katibu wa CCM mkoa wa
Kilimanjaro Jonathan Mabihya, akiongoza Kamati ya Siasa kukagua na kutembelea
mradi wa ujenzi wa maji Njoro II uliopo Wilaya ya Rombo.
0 Comments:
Post a Comment