Saturday, February 15, 2020

Watendaji wa Umma Siha watakiwa kuishi maeneo ya kazi

Watendaji katika Sekta ya Umma, wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, watakiwa kuishi maeneo yao wanayofanyia kazi  ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Omari Kisesa, wakati wakitoa msaada wa mifuko 30 ya saruji kwa  ajili ya kuchangia ujenzi wa kituo  kipya cha polisi wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa kimsingi utumishi wa umma huendeshwa kwa misingi yake, Ofisi za Umma haziendeshwi kama tunavyoendesha familia zetu, ni ofisi ambayo ina misingi na miongozo yake huku akiwasisitiza watumishi wa umma kuishi katika maeneo yao ya kazi  wanapofanyia.

“Wapo  baadhi  ya watumishi wa umma wanafanya kazi katika halmashauri ya wilaya ya Siha, lakini inapofika jioni kulazimika kwenda Moshi na Hai na wengine wanaishi Jijini Arusha jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utumishi bora,”alisema Kisesa.

Alisema watumishi wa umma wanatakiwa kuishi katika maeneo yao ya kazi na kwamba jambo hilo lilishazungumzwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira pamoja na Mkuu wa wilaya ya Siha Onesmo Buswelu lakini linaonekana jambo hili halijatekerlezwa vya kutosha.

“Naomba kuwakumbusha tena  watumishi  umma wanaoishi nje ya wilaya hii warudi na kuishi katika eneo lao la kazi,  wapo baadhi ya watumishi wa umma wanaishi  wilaya ya Moshi, Jijini Arusha na wengine wanaishi katika wilaya Hai, lakini viongozi wenu wote akiwemo Mkuu wa wilaya na Mkurungenzi mtendaji wanaishi ndani ya wilaya sasa inakuwaje ninyi  watendaji wa halmashauri kuishi nje ya kituo chenu cha kazi??alihoji Kisesa.

Awali  mkuu wa kituo cha polisi Siha Namsemba Mwakatobe, alisema kuwa majengo wanayotumia kwa sasa yana changamoto nyingi  ikiwemo uchakavu wa  mfumo wa maji taka pia majengo ni machache hayakidhi mahitaji ikiwemo chumba cha mahabusu ya watoto wa kiume  na yale ya  watoto wa kike.

“Jengo  hili litakapo kamilika litakuwa na mahitaji yote muhimu  ikiwemo sehemu ya kuhifadhia silaha, ofisi ya mkuu wa kituo, upelelezi , eneo la kutunzia vielelezo mbalimbali, eneo la ukumbi wa mikutano, ofisi ya dawati na ofisi zote ambazo ni sehemu ya jeshi la polisi kwa ngazi ya wilaya zitakuwepo,”alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Onesmo Buswelu, aliwataka wananchi kuendelee kuchangia ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.

Buswelu alisema ujenzi huo kwa sasa upo katika hatua za awali za ujenzi wa msingi na kuonya wale waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi huo wasifanye ujanja ujanja kwa kuiba nondo na sementi  kwani sheria itachukua mkondo wake.

“Kituo kilichopo  kilijengwa enzi za wakoloni, hivyo majengo yake  yamechakaa licha ya kwamba tuliendelea kuyatumia kama kituo cha polisi, kwa sasa tunakwenda kuanza ujenzi wenye miundombinu ya kisasa inayoendana na mahitaji ya jeshi la polisi na ujenzi huu unatarajia kugharimu zaidi ya  cha Sh milioni 270,”alisema DC Buswelu.

STORY BY: Kija Elias, Siha.........................................................Februari 15, 2020

0 Comments:

Post a Comment