Tuesday, February 11, 2020

Auawa kwa kuchinja kitoto cha mbuzi

MKAZI wa Njiapanda, aliyefahamika kwa jina la Samweli Mkata (35) amefariki dunia kwa kukatwa na panga kwa kile kinachodaiwa kuchinja kitoto cha mbuzi aliyetoka kuzaa.

Mashuhuda wa tukio hili walisema tukio hilo lilitokea Februari 5 mwaka huu baada ya muuaji aliyefahamika kwa jina la Ganzi Mkata (32) kumkata kwa panga baada ya kutokea sintofahamu kuhusu kitoto hicho cha mbuzi.

Wawili hao ni ndugu wa tumbo moja muuaji ni mdogo wa marehemu ambaye siku ya tukio alibaini kuwa kitoto cha mbuzi hakipo baada ya kuuliza akaambiwa kuwa kaka yake ambaye ni marehemu ndiye aliyekichinja.

"Yaani inasikitisha mdogo mtu alipoona kitangana (kitoto cha mbuzi) hakipo aliuliza na kuambiwa kuwa kaka yake (Samweli) amekichinja na kumpatia mbwa, ndipo alipoapa kuwa lazima amuue aliyefanya hivi, tukajua utani tu," alisema mmoja wa ndugu wa marehemu.

Baada ya muuaji kusema hayo alianza kumtafuta kaka yake majira ya saa tatu asubuhi ambapo watu walisikia kelele za ugomvi na kwamba mdogo mtu anapambana na marehemu.

Hatimaye marehemu alizidiwa nguvu na muuaji kisha kuanguka chini wakati ndugu, jamaa na marafiki walipofika kuamulia ugomvi huo.

"Damu zilikuwa zikichuruzika katika eneo la shingo, tukatafuta kanga ili kuzuia damu hiyo na kumwahisha hospitalini," alisema shuhuda za tukio hilo.

Marehemu alikata roho baada ya kufikishwa katika hospitali ya Himo maarufu Kwa Minja, mjini Moshi.

Diwani wa Kata ya Njiapanda Aloyce James Mboya alisema ndugu hao hawakuwa na ugomvi wa aina yoyote isipokuwa ni akili za kitoto za muuaji kwani kaka mtu alikiona kitoto cha mbuzi kuwa hakitakuwa na maisha marefu kutokana na kuwa dhaifu tangu siku ya kwanza.

Jeshi la Polisi limethibitisha kumshikilia mtuhumiwa mauaji hayo na kidhibiti ambacho ni panga tayari kwenda naye mahakamani kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili.

0 Comments:

Post a Comment