Thursday, February 27, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Boris Nemtsov ni nani?

Februari 27, 2015 alifariki dunia mwanasayansi na mwanasiasa wa Russia Boris Yefimovich Nemtsov. Nemtsov alikuwa mtaalamu wa Fizikia. 

Katika siasa alikuwa kiungo muhimu katika kuanzisha ubepari katika ardhi ya Usovieti. 

Alifanikiwa sana katika masuala ya siasa miaka ya 1990 wakati wa utawala wa Rais Boris Yeltsin. 
Kuanza mwaka 2000 hadi kifo chake alikuwa mpinzani wa Vladimiri Putin. 

Mwanasiasa huyo alichapwa risasi nne kutoka mgongoni mbele ya mpenzi wake raia wa Ukraine, Anna Duritskaya. 

Majuma kadhaa kabla ya kuuawa kwake Nemtsov alielezea hofu yake kwa Putin kwamba anaweza kumuua. 

Miaka miwili baadaye watu watano wa Chechnya walikamatwa na kukutwa na hatia na mahakama ya haki ya Moscow baada ya kukubali kuwa walikubaliana kufanya mauaji hayo kwa kiasi cha dola la Kimarekani 253,000 ambazo ni sawa na Shilingi milioni 585 za Tanzania. 

Hata hivyo hakuna mtu anayedaiwa kuwakodi watu hao kufanya mauaji. 

Nemtsov alikuwa akiikosoa serikali ya Putin kuwa imekuwa ya kibabe, isiyo na demokrasia, matumizi mabaya ya fedha kuelekea michuano ya Olimpiki ya Sochi na Uingiliaji wa kijeshi katika ardhi ya Ukraine. 

Baada ya mwaka 2008 Nemtsov alichapisha kwa kina ripoti kuhusu rushwa kwenye serikali ya Putin. 

Ikiwa ni sehemu ya mapambano ya siasa Nemtsov aliendelea kuwa mratibu wa maandamano ya Raia wa Russia wakipinga mswada uliouitwa Straregy 31. 

Maandamano hayo yalikuwa yakitaka uchaguzi huru ufanyike kwa tume huru. 

Wakati anauawa Nemtsov alikuwa jijini Moscow akijaribu kuratibu kundi la watu kwa ajili ya kuvipinga vikosi ya kijeshi vya Russia kutokana na mgogoro wa Ukraine na Russia. 

Pia Nemtsov kabla ya kuuawa alikuwa njiani kuandika ripoti kuhusu namna majeshi ya Russia yalivyokuwa yakipigana na wanajeshi wa zamani wa Russia katika ardhi ya Ukraine, taarifa ambazo Kremlin ilikuwa inazikataa. 

Taarifa hizo zilikuwa hazifahamika ndani na nje ya Russia. 

Nemtsov alikuwa gavana wa kwanza wa Nizhny Novgorod Oblast kutoka mwaka 1991 hadi 1997. Baadaye alifanya kazi na serikali ya Russia akiwa Mafuta na Nishati mwaka 1997. 

Pia Nemtsov alikuwa Makamu wa Baraza la Usalama la Russia kutoka mwaka 1997 hadi 1998. Miaka iliyofuata alijiingiza katika kuunda vikundi vya kisiasa. 

Hadi mauti yanamkuta Nemtsov alikuwa miongoni mwa viongozi wa Vuguvugu la Solidarnost (Mshikamano) na mbunge wa bunge la mkoa wa Yaroslavl Oblast na makamu mwenyekiti wa chama cha RPR-PARNAS. 

Baada ya mauaji hayo mwandishi Serge Schmemann wa gazeti la New York Times aliomboleza kifo cha mwanasiasa huyo, kwa kuandika, "A Reformer Who Never Backed Down."  

Pia mwandishi huo aliongeza "Tall, handsome, witty and irreverent, Mr. Nemtsov was one of the brilliant young men who burst onto the Russian stage at that exciting moment when Communist rule collapsed and a new era seemed imminent." 

Ikiwa na maana ya "Mrefu, mzuri, mwerevu na asiye na heshima, Nemtsov alikuwa mmoja wa vijana wenye busara ambao waliibuka Nchini Urusi katika hatua Ukomunisti ulipokuwa ukifikia zama zake za mwisho."

Nemtsov alizaliwa Oktoba 9, 1959 Sochi nchini Russia na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 55.

0 Comments:

Post a Comment