Friday, February 7, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Papa Pius wa IX ni nani?

Februari 7, 1878 alifariki dunia Kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Pius wa IX. Papa huyo aliliongoza kanisa hilo kutoka Juni 16, 1846 hadi mauti yake. 

Aidha Papa Pius wa IX anasalia kuwa ni kiongozi wa juu wa kanisa hilo kukalia wadhifa huo kwa muda mrefu akihudumu kwa muda wa miaka 31. Papa Pius wa IX alishika wadhifa huo baada ya kifo cha Papa Gregory wa XVI aliyeliongoza kanisa hilo kutoka mwaka 1831 hadi 1846. 

Wakati wa utawala wake Papa Pius XI alikuwa maarufu sana nchini Italia kutokana na sera zake za kiliberali. Pia alifanikiwa kumpa mamlaka Waziri Rossi kufanya kazi zake za kiutawala katika viunga vya himaya yake ya Upapa. 

Papa Pius wa IX alionyesha wazi kuwa yupo kinyume na sera la Austria ambapo wazalendo wa Italia walimuona kama mkombozi kwao. 

Kama haitoshi wakati wa utawala wake alifanikiwa  kuboresha kilimo kwa kuingiza teknolojia za kisasa na elimu kwa wakulima ikiwamo kuanzisha taasisi za kilimo. Papa Pius wa IX alifariki kwa ugonjwa wa kifafa na maradhi ya moyo.

Alizaliwa Mei 13, 1792 huko Senigallia. Jina lake halisi ni Giovanni Maria Mastai Ferretti. Alikuwa mtoto wa tisa wa familia ya kitajiri ya Girolamo dei conti  Ferretti. 

Alibatizwa siku hiyo hiyo  baada ya kuzaliwa na kupewa jina Giovanni Maria Battista Pietro Pellegrino Isidoro.  Alipata elimu yake  katika chuo cha Volterra na Rome. 

Akiwa kijana akiwa Guardila Nobile alihusika katika jaribio la kutaka kumwoa mwanamke raia wa Ireland Miss Foster  ambaye alikuwa binti wa Askofu wa Kilmore. 

Mipango ya harusi iliwekwa sawa na kwamba harusi hiyo itafungiwa katika Kanisa la Mtakatifu Luigi Del Francesi. Wazazi wake walipinga suala hilo  na hata siku ya tukio lakufunga harusi kanisani hawakuweza kutokea. 

Akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Theolojia katika mji wa nyumbani,  Giovanni Ferretti alikutana na Papa Pius wa VII wakati akirudi kutoka makucha ya Wafaransa walikokuwa wametekwa. Hiyo ilikuwa mwaka 1814. 

Mwaka mmoja baadaye Giovanni Ferretti aliingia na kuwa miongoni mwa kikosi cha walinzi wa Papa. Lakini huko hakufanikiwa kukaa kutokana na kuwa na dalili za kuwa na ugonjwa wa kifafa. 

Alimwangukia miguu Papa Pius wa VII ambaye ndiye alimpa msaada mkubwa wa kuendelea na masomo ya theolojia.


0 Comments:

Post a Comment