Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania (KLFT) Jones Molla. |
Waumini na wananchi wote, wakiwemo wenye dhamana za uongozi wameshauriwa kuepuka chuki ili amani iliyopo kwenye kanisa, taifa na ulimwenguni iendelee kuwepo.
Mbali na kukosekana kwa amani pia chuki huzaa ukandamizaji ndani ya jamii, jambo ambalo linasababisha kutokuelewana miongoni mwa wanajamii kutokana na mvutano unaotokea kati ya wale wanaokandamizwa na wanaodaiwa kuwakandamiza wenzao.
Ushauri huo umetolewa jana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania (KLFT) Jones Molla, wakati akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada ya mazishi ya John Simbo Shuma, iliyofanyika katika Kanisa la Kiluther Tanzania (KKKT) Usharika wa Machame Nkwarungo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Askofu Molla alisema mbali na kuwepo chuki zinazohatarisha amani katika ngazi hizo alisema pia kuna chuki katika ngazi ya familia ambayo ndiyo imekuwa chanzo cha kurithisha chuki kwa kizazi kijacho.
Aidha katika salamu zake hizo za pole Askofu Molla, aliwataka waumini kusimama imara katika imani na dini zao, na kujiepusha kukimbilia miujiza ambayo wamekuwa wakiahidiwa huko, huku wakiambulia matatizo tofauti na walivyotarajia.
“Ndugu zangu ninawasihi sana acheni kutanga tanga huku na kule kwa kufuata mafundisho mbalimbali yanayotolewa na makanisa ambayo yameanza kuibuka ili kuepusha na madhara yanayojitokeza, simameni katika imani zenu huku mkimuomba Mungu kwani lipo tumaini kwake hakika atawashindia,”alisema Askofu Molla.
Hata hivyo Askofu Molla aliwataka watumishi ambao wamekuwa wakitumia mahitaji ya watu kuwa mtaji wao kwa kuwataka kupeleka udongo, vitambaa, maji, ili vikaombewe wapate fedha kuacha tabia hizo.
“Ninawasihi sana Watumishi wa Mungu kamwe tusitumie uhitaji wa watu kuwa mtaji wetu kwani ni dhambi kuumiza watu ninawasihi wahubirini watu kwa kulisoma neon la Mungu Zaidi,”alisema.
STORY BY: Kija Elias, Moshi.......................Februari 11, 2020
0 Comments:
Post a Comment