Mahakama ya Mwanzo ya Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro imemhukumu kifungo cha miezi sita jela kijana anayesadikiwa kuwa ni mwizi na tapeli sugu wa makapeti ya bajaji.
Hayo yamejiri baada ya mlalamikaji aliyefahamika kwa jina la Aminiel Daudi Mongi mwenye umri wa miaka 62, mfanyabiashara na mkazi wa Bonite, Chekereni mjini Moshi kuithibitishia mahakama pasipo shaka yoyote kuhusu namna wizi huo ulivyotokea.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Adnan Kingazi alisema mshtakiwa Jacobo John Chilla miaka umri wa miaka 25, Mkazi wa Soweto Moshi, Kondakta wa Hiace za Soweto alikiuka kifungu cha sheria Na. 265 cha Makosa ya Jina , Sura ya 16 ya Kanuni ya Adhabu.
Awali ilidaiwa mahakamani kuwa Novemba 28, 2019 majira ya saa 8:00 mchana maeneo ya kota za polisi, Manispaa ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro mshtakiwa kwa makusudi na bila halali huku akifahamu kuwa ni kosa aliiba carpet ya Bajaji mali ya mlalamikaji, yenye thamani ya Tshs. 50,000/= kitendo ambacho ni kosa na kinyume cha sheria.
Mshtakiwa aliposomewa alikana shtaka hilo na ndipo mahakama ilipoamua kujidhirisha kwa kupeleka mashahidi.
Mlalamikaji aliiambia Mahakama namna alivyoibiwa capeti ya bajaji yake na mshtakiwa aliyekuwa amempakiza kama abiria.
Ushahidi ulionyesha kuwa mshtakiwa alionekana na askari mwenye namba F.2158 SGT Pius aliyekuwa eneo la line polisi ambapo aliwasimamisha na kumwamuru mshtakiwa aokote uchafu wake ambao kwa wakati huo hakujua kuwa ni kapeti la mlalamikaji.
Mshtakiwa huku akijua alichokifanya aliokota kapeti ile na kuelekea kusikojulikana kwa lengo la kuiuza.
Hadi baadae mlalamikaji alipogundua kuibiwa capeti yake na kutoa taarifa kituo cha polisi hadi mshtakiwa alipokamatwa na kufunguliwa shauri hili.
Mahakama ilitafakari kwa kina ushahidi wote wa pande zote mbili na kujiuliza baadhi ya hoja za msingi sana Kwamba je, viini halisi vinavyounda shtaka la wizi vimetimia?
Hoja ya pili ni kwamba je, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka la wizi dhidi ya mshtakiwa katika kiwango kinachostahili cha kutokuacha chembe ya shaka?
Katika kujibu hoja hizo mbili mahakama ilijikita zaidi katika ushahidi uliotolewa pande zote mbili, na kuthibitisha shtaka lolote la jinai kisheria lazima kuthibitisha viini halisi viwili ambavyo ni nia ovu na tendo ovu la mshtakiwa.
Lakini pia kila shtaka la jinai limeundwa na viini vyake halisi.
Mahakama ilisema kwenye shtaka la wizi viini vyake ni asportation, yaani kuhamishwa kwa mali husika kutoka sehemu moja hadi nyingine, pia mali iliyoibiwa lazima iwe na mwenyewe na pia iwe na thamani na yote hayo yalitimia katika kesi hiyo.
Kingazi alisema ushahidi wa upande wa mashtaka ulionyesha kufanana kwa kiasi kikubwa na kubwa zaidi lililoonekana ni kwamba mshtakiwa alionekana akitupa kitu chenye uzito ambacho baadae ilifahamika kuwa ni kapeti ya mlalamikiaji huku akiwa na lengo la kuifuata baadae aichukue aiuze ili ajipatie kipato.
Mshtakiwa alikiri hilo katika utetezi wake kuwa alitupa kitu hicho alichodai kuwa ni uchafu wa karatasi ya nailoni uliokuwa unamkera ndani ya bajaji.
Hakimu Mkazi Kingazi alisema Mahakama iliridhika pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitupa kapeti na siyo nailoni kama alivyodai kwani ushahidi ulithibitisha wazi kitu alichotupa ilikuwa ni mali ya wizi.
Pia ilielezwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa amekuwa akitafutwa kwa makosa ya aina hiyo hiyo kwa muda mrefu kwani amekuwa ni mhalifu wa kapeti za bajaji mjini Moshi na amekuwa ni kero kubwa.
Mshtakiwa alikiri kosa na kuomba apewe muda akamlipe mlalamikaji kapeti lake na aliahidi kuwa raia mwema endapo atapata msamaha wa mahakama.
Wakati wa utetezi wake mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzi adhabu kwa vile anaishi na babu yake ambaye ni mzee sana na kwamba anaumwa na anatumia mpira puani.
Pia mshtakiwa aliiambia mahakama kuwa amekuwa akimlisha kila baada ya saa sita na kwamba familia yao haina uwezo.
Hivyo mahakama kwa kusikiliza utetezi wake iliona kuna haja ya kumpungizia adhabu kutokana na maombolezo aliyoyatoa
Nchini Tanzania kwa mujibu wa kifungu na 3(2) (a) cha Sheria ya Huduma kwa Jamii ya mwaka 2002 kifungo cha nje ni utaratibu ambao unampa fursa mfungwa kutumikia kifungo chake nje ya gereza kwa kufanya shughuli/kazi zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii.
Utaratibu huu hutolewa kwa wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miaka mitatu bila kujali wana faini au hawana.
Wapo wahalifu wanaohukumiwa moja kwa moja mahakamani kwenda kutumikia kifungo cha nje na wengine huingia gerezani kwanza na baadaye utaratibu wa maombi maalum hufanyika ili mfungwa husika kwenda kutumikia kifungo kwa utaratibu huo.
Sheria ya Magereza Sura ya 58 kifungu Na. 52 (1) (2) inatoa utaratibu wa kumuondoa mfungwa aliyepo gerezani huku akiwa ana sifa ya kutumikia kifungo chake kwa utaratibu wa huduma kwa jamii.
Kifungu hicho cha Sheria kinaeleza kuwa pale ambapo Mkuu wa gereza atajiridhisha kuwa kuna mfungwa ambaye ana sifa ya kutumikia kifungo chake chini ya utaratibu wa huduma kwa jamii, atamshauri mfungwa huyo juu ya utaratibu huo kwa kuzingatia sifa alizonazo na ikiwa mfungwa huyo ataridhia kuachiliwa kwake katika utaratibu wa huduma kwa jamii, Mkuu wa Gereza atawasilisha maombi maalum katika Mahakama iliyomfunga kwa ajili ya maandalizi ya kuachiliwa kwa mfungwa huyo katika utaratibu wa huduma kwa jamii.
Mfungwa anayetumikia kifungo cha nje ni lazima aishi kwa kufuata Sheria na masharti aliyopangiwa. Masharti hayo ni kuwa chini ya uangalizi maalum, kutoondoka nje ya Mkoa bila kibali na kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka muda wake wa kifungo chake utakapokamilika.
STORY BY: Jabir Johnson............................Feb 20, 2020
0 Comments:
Post a Comment