Saturday, February 15, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Maria Elena Moyano Delgado


Februari 15, 1992 alifariki dunia mwanaharakati mweusi wa nchini Peru; María Elena Moyano Delgado.

Mwanamke huyo alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 33. Maria aliuawa na kundi la watu wenye msimamo mkali nchini Peru lenye siasa za Kimao lililofahamika kwa jina la Sendero Luminoso.

Kundi hili lilikuwa la kigaidi lilianza kuweka misimamo ya kutaka kuiangusha demokrasia mpya katika taifa hilo na kuweka sera mpya ya udikteta.

Aidha kundi hilo lililaumiwa sana kwa ukatili wake dhidi ya Wakulima, Wafanyabiashara, maofisa wa serikali waliochaguliwa na jamii kwa ujumla. 

Lilianzishwa mnamo mwaka 1980 na kusambaa katika nchi mbalimbali zikiwamo Peru, Marekani, Japan, Canada na Umoja wa Ulaya.

Kundi hilo lilipoteza nguvu nchini Peru mnamo mwaka 1992 wakati ambapo kiongozi wao mkuu Abimael  Guzman aliposhikwa na serikali ya Peru ambayo ilimhukumu kifungo cha maisha jela.  

Sababu ya kifo cha mwanaharakati huyo ni kutofautiana na waliokuwa wakifuata msimamo wa Mao ambao kwa kiingereza walikuwa wakiijita Shining Path.

Baada ya hapo mwanaharakati Maria Delgado alianza kutabiri kuhusu kifo chake kwani hapo awali wanaharakati wawili nchii Peru waliuawa ma kundi hilo hilo.

Maria Antenati Hilario na Margarita Astride de la Cruz walikuwa miongoni mwa wanaharakati waliouawa wakati huo na akiamini kuwa zamu yake itafika.

Pia mauaji ya mwanaharakati muhimu nchini humo Juana Lopez mwaka 1991 kilimfanya Maria Delgado kujua kuwa zamu yake ilikuwa inafuata. Mwanaharakati alianza kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa kundi hilo endapo asingekubali matakwa yao.

Februari 14, 1992 wanajeshi wa kundi la Shining Path waliingia mjini Lima ambako ni makao makuu ya Peru na siku hiyo hiyo mwanaharakati Maria Delgado alikuwa amepanga maandamano akiwakusanya wanawake kupinga ugaidi.

Kiuhalisia Shining Path hawakuingia kwa ajili yake mjini humo lakini jaribio lao lilishindikana kwani walipata upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa jamii mjini humo.

Februari 15, 1992 Maria Delgado alikuwa akisherekea kumbukizi ya kuzaliwa kwa mtoto wake wa kiume katika mgahawa mmoja uliokuwa kwenye ufukwe wa bahari ndipo wanaume na wanawake waliokuwa na silaha walipomzingira wakati akitoka nje ya mgahawa huo na kumkamata.

Akiwa mikononi mwa wanajeshi hao wa Shining Path alitokea mwanamke mmoja akiwa na silaha na kumtandika risasi za kutosha  mbele ya watu waliokuwepo ufukweni hapo.

Mwanaharakati huyo alijua kuwa wanajeshi hao walikuwapo ufukweni hapo kwa ajili yake na sio vinginevyo hivyo hakuwa na hofu kwani alishajua siku nyingi kuwa zamu yake ya kifo imewadia.

Alitandikwa risasi mbele ya mtoto wake wa kiume na mumewe David Pineki aliyekuwa naye tangu mwaka 1980. Mwili wake ulichukuliwa na wanajeshi hao hadi katikati ya viunga vya mjini Lima na kulipuliwa huko kwa baruti. Ilikuwa huzuni Peru yote kutokana na mauaji ya mwanaharakati huyo mtetezi wa wanawake na jamii ya Peru.

Maelfu walihudhuria mazishi yake. Sanamu ya mwanaharakati Maria Delgado ilisimamishwa katikati kitongoji cha Villa El Salvador jijini Lima na wasifu wake ulisomwa hapo.

Mauaji ya Maria Delgado yalikuwa ya mwisho yaliyofanywa na kundi la Shining Path. 

Mwanaharakati huyo alipewa heshima kupitia filamu baada ya kifo chake iliyopewa jina la Coraje (Courage) iliyoongozwa na Alberto Durant.

Taifa la Peru lililojawa na vurugu, kukosekana kwa usawa na hatari mbalimbali Maria Elena Moyano Delgado alionyesha kuwa ni tumaini la watu hao na hiyo ilijidhihirisha wakati wa mazishi yake ambapo watu akali ya 300,000 walipohudhuria.

Maria Delgado alizaliwa Novemba 29, 1958 huko Barranco mjini Lima. Alianza harakati zake tangu akiwa kijana akiwa na kundi la Movimiento de Jóvenes Pobladores huko Villa El Salvador kitongoji ambacho kilikuwa kikikaliwa na watu kutoka vijijini.

0 Comments:

Post a Comment