Tuesday, February 11, 2020

Utalii wa Michezo: Medani ya Utalii isiyopewa kipaumbele

Mwanariadha wa Tanzania Alphonce Felix Simbu ni miongoni mwa wanariadha ambao wamekuwa wakifanya utalii wa michezo pindi anapokwenda kukimbia mbio mbalimbali duniani. Mnamo mwaka 2016 alishika nafasi ya tano katika michuano ya Olimpiki jijini Rio de Janeiro katika marathon alipomaliza kwa saa 2:11.15.
Inafahamika kwa kila mmoja wetu linaposikika neno 'Utalii' katika masikio watu hususani Watanzania. 

Kwa ufupi ni kwamba utalii ni kusafiri kwa ajili ya burudani, burudani makusudi au biashara.

Pia utalii huweza kukuza uchumi wa nchi fulani endapo nchi hiyo itapokea fedha za kigeni kutoka kwa watalii ambao wanatoka nchi tofauti na nchi hiyo ambayo imepokea fedha za kigeni.

Karne moja hivi iliyopita, watu wengi duniani hawakuwa wakienda likizo kwa ukawaida. 

Na zaidi, watu wengi walikaa karibu na kwao maisha yao yote bila kutembelea maeneo ya mbali. 
Kusafiri nchi za mbali ili kustarehe au kujielimisha kulikuwa jambo la pekee na ni watu wachache tu matajiri au waliopenda kusafiri ambao waliweza kufanya hivyo. 

Lakini siku hizi, mamia ya maelfu ya watu wanaweza kusafiri kokote katika nchi yao au hata ulimwenguni. 

Sababu kubwa ya mabadiliko hayo ni yale maendeleo makubwa ya kiviwanda, mamilioni ya watu waliajiriwa kazi za kutengeneza bidhaa na kutoa huduma. 

Matokeo yakawa kwamba watu walichuma mapato mengi. Kwa sababu ya maendeleo ya tekinolojia, mashine zilibuniwa nazo zilipunguza kazi na gharama. 

Hivyo, watu wengi walipata wasaa wa kustarehe. Kwa kuongezea mambo hayo, usafiri wa umma wa bei nafuu ulipoanzishwa katikati ya miaka ya 1900, biashara ya utalii ilisitawi. 

Kisha, matangazo ya televisheni yaliyokuwa tu yametoka kuanzishwa, yaliwachochea watu kusafiri kwa kuwaonyesha watu ulimwenguni pote picha za maeneo ya mbali wakiwa nyumbani mwao.

KIBO SPORTS CLUB KUINUA UTALII WA MICHEZO
Hadi sasa nchini Tanzania kumekuwa na idadi kubwa ya watalii wanaoingia kila mwaka kwa ajili ya kutazama, kujielimisha kuhusu vivutio vingi kama wanyama, mbuga, milima na kadhalika.

Mkoani Kilimanjaro kumekuwa na vivutio vingi ukiwamo mlima mrefu kuliko yote barani Afrika Mlima Kilimanjaro.

Hata hivyo licha ya vivutio vingi ambavyo kila mmoja amekuwa akidhani hivyo utalii wa michezo umesahaulika katika ardhi ya Tanzania ukionekana kuwa sio utalii bali ni kama fani nyingine tu.

Makala haya yamezungumza na Mkurugenzi wa Kibo Sports Club Daniel Mvungi anayetazama utalii wa michezo kama fursa muhimu kwa watalii wanaotoka nje ya Tanzania.

Mvungi anaungana na waandishi watatu (Gammon,Robinson na Gibson ) waliojaribu kutafsiri maana halisi ya utalii wa Michezo katika vipengele tofauti.

"Utalii laini wa Kimichezo ni wakati ambapo mtalii anajihusisha na michezo kama mbio, kusafiri na mtumbwi kwa huku kwetu Tanzania," anasema Mvungi.

Pia Mvungi anakubaliana Utalii Ulio Hai wa Michezo (Active Sports Tourism) ambao unahusisha watu ambao wanashiriki matukio ya kimichezo.

"Mwaka huu tunashuhudia tena kwa mara nyingine Kilimanjaro Marathon ikifanyika katika mkoa wetu. Hiyo yote ni utalii huu wa michezo kwani ni muda mrefu sasa mbio hizo zinafanyika hivyo wanariadha mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali wanapokuja kukimbia wanafanya utalii wa michezo ulio hao," anaongeza Mvungi.

Aidha Mvungi anasema kuna aina nyingine ya utalii wa michezo ambao unahusisha watu wanaokuja kutazama tu, kitaalamu unafahamika Sports Event Tourism ambao mara kadhaa huweza kufanyika kwa muda fulani kama Kombe la Dunia katika mchezo wa Soka au michuano ya Olimpiki.

Kwa kuonyesha azma ya kufufua Utalii wa Michezo mkoani Kilimanjaro Mvungi anasema wameanzisha Triathlon ambayo watajumuisha michezo mitatu ikiwamo mbio (running), kupanda mlima (climbing) na Safari & Beach Holiday kwenda Zanzibar.

"Tutatumia mbio hizi za Kili Marathon 2020 ambazo zimekuwa maarufu sasa ndani na nje ya Tanzania kufanya utalii huu kupitia hii Triathlon. Wale watalii ambao tutakuwa tumezungumza nao watakapofika tutawapokea na kuwatambua kisha kuingia katika ushiriki huo," anasema Mvungi.

Mvungi anasisitiza kuwa utalii huo mwaka huu watashirikiana na watu wengine ambao wapo kwenye medani ya utalii kwa muda mrefu sasa ili kuhakikisha watalii wataofika wafurahie kama ilivyo nia thabiti ya michezo.

FAIDA ZA UTALII WA MICHEZO
Ili kuonyesha jinsi utalii unavyoweza kuboresha uchumi wa nchi, fikiria Visiwa vya Bahamas, taifa dogo la visiwa vilivyo karibu na Ghuba ya Mexico kati ya jimbo la Florida huko Marekani na kisiwa cha Cuba. 

Visiwa vya Bahamas havina mali ghafi nyingi wala wenyeji wake hawafanyi ukulima kwa kadiri kubwa. Lakini visiwa hivyo huwa na halihewa yenye joto, pwani safi za tropiki, wakazi wenye urafiki wapatao 250,000, na viko karibu na Marekani. 

Utalii hufaidi wahusika wote. Mtalii anapotembelea nchi ya kigeni yeye hutumbuizwa au kuelimishwa.

Utalii wa michezo kimataifa huwezesha nchi hizo kupata fedha za kigeni. Nchi nyingi huhitaji fedha za kigeni ili kulipia huduma na bidhaa zinazotoka katika nchi nyingine.

Mapato ya serikali yanayochumwa kutokana na utalii yanatumiwa kuboresha mifumo ya umma, viwango vya elimu, na kutimiza mahitaji mengine makubwa ya taifa. 

Karibu serikali zote hutaka raia wake wawe na kazi ya kuajiriwa. Utalii husaidia kutokeza kazi za kuajiriwa.

Imetayarishwa na Jabir Johnson, Moshi..............Februari 11, 2020. Kwa maoni, ushauri baruapepe: johnsonjabir@gmail.com 

0 Comments:

Post a Comment