Februari 8, 2018 alifariki dunia msanii wa muziki wa Ghana mwanadada maarufu Ebony Reigns. Jina lake halisi ni Priscilla Opoku-Kwarteng.
Nyota huyo wa muziki wa Dancehall na hiplife alifariki dunia kwa ajali mbaya ya gari iliyotokea jijini Accra.
Alipoteza maisha katika ajali hiyo akitokea Sunyani alikokwenda kumsalimia mama yake. Msaidizi wake na rafiki yake wa siku nyingi Franklina Yaa Nkansah na askari Atsu Vondee walipoteza maisha katika ajali hiyo.
Aliyepona katika ajali hiyo ni dereva wa gari hilo.
Ebony Reigns kama alivyokuwa akijulikana akiwa jukwaani alifariki dunia siku nane kabla ya kutimiza miaka 21 ya kuzaliwa kwake.
Taratibu za mazishi zilifanywa mbele ya viunga vya Ikulu jijini Accra ana alizikwa katika makaburi ya Osu Jumamosi ya Machi 24, 2018.
Familia ya Ebony ilipata rambirambi nyingi kutoka kwa watu maarufu, serikali na taasisi binafsi.
Kifo cha msanii huyo kilizua utata na taifa la Ghana liligawanyika.
Kuna wale walioamini kuwa ajali hiyo isingetokea kama barabara zingekuwa zimetengenezwa vizuri na kuwa na taa.
Barabara ya Mankranso ambayo ndio ajali hiyo ilitokea usiku wa siku ya tukio ilikuwa katika hali mbaya hususani nyakati za usiku.
Upande mwingine uliamini kuwa kifo cha Ebony Reigns ilikuwa ni mipango ya Mungu japokuwa kilikuwa katika hali ya kuogofya hivyo basi kama ni Mwenyezi Mungu huwezi kuzuia.
Hata hivyo kuna wengine hususani viongozi wa dini wachungaji na wainjilisti walidai kuwa kifo cha mwanadada huyo ni kutimizwa kwa unabii kwa waliwahi kutabiri kuwa asipobadili muundo wa maisha yake hakika angekufa.
Mchungaji maarufu sana nchini Ghana Dkt. Lawrence Tetteh alizungumzia kuhusu baadhi ya wanamuziki na wafanyabiashara kuwa kupitia kifo cha Ebony Reigns walianza kujinufaisha.
Hilo lilijidhihirisha pale Kampuni moja la nguo nchini Ghana la GTP lilipotengeneza nguo zikiambatanisha na nyimbo kali za Aseda na Maame Hw3 kwa ajili ya sherehe za harusi na mazishi.
Mchungaji huyo alidai kuwa walitumia kiasi kikubwa cha fedha katika mazishi kuandaa mazishi ya msanii huyo licha ya kwamba ilikuwa ni vigumu kuamini hilo.
Maneno ya Mchungaji huyo yalizua utata zaidi kwasababu baadhi ya watu walisema kuwa mchungaji huyo hakupaswa kujihusisha na hilo au kuelezea maoni yake katika mitandao ya kijamii. Aidha kifo cha Ebony kilisababisha nchini Ghana kuibuka unabii wa kila aina kuhusu vifo vya wasanii wengine akiwamo Shatta Wale kwamba atafariki kabla ya Desemba 25, 2018 na kuongeza kwamba manabii hao wanao uwezo wa kuzuia visitokee.
Hata hivyo wengi hawakuamini hilo lakini walistaajabishwa pale msanii huyo namba moja wa kategori ya dancehall nchiini humo alipotoa vitisho kupitia video moja kuwa endapo hatakufa tarehe iliyotajwa basi atachoma moto baadhi ya makanisa nchini humo.
Vyanzo mbalimbali vilikaririwa vikitoa maoni yake kuwa kifo cha Ebony Reigns kila mmoja ana haki ya kuamini kulingana na moyo wake ulivyomtuma.
Baada ya kifo cha msanii huyo baadhi ya wasanii nchini Ghana akiwamo Sarkodie na Stonebwoy walianza kampeni ya usalama barabarani ili kupunguza idadi ya vifo vinavyotokea kutokana na ajali za barabarani.
Mwaka mmoja baada ya kifo chake raia wengi wa Ghana walionyesha upendo na kumbukizi ya kifo cha nyota huyo wa dancehall kwa kuweka picha za Ebony Reigns katika mitandao ya kijamii huku wakitoa rambirambi zao.
Sarkodie aliachia wimbo unaofahamika kwa jina la "Wake Up Call" akionyesha vyanzo mbalimbali vya ajali za barabarani na namna ya kupunguza ajali hizo. Katika wimbo huo alimshirikisha msanii mwingine anayefahamika kwa jina la Benji wakiitaka serikali kutengeneza barabara na wakisisitiza polisi ya nchi hiyo kusimamia sheria za usalama barabarani.
Wizara ya Utalii, Utamaduni na Sanaa Bunifu ya taifa hiyo iliunga mkono kampeni hiyo.
Enzi za uhai wake Ebony alishinda tuzo tofauti saba zikiwamo People's Celebrity mnamo mwaka 2017 na Vodafone Ghana Music mwaka 2016 na 2018.
Ebony alizaliwa Februari 16, 1997 huki Oheema zamani Nana Heemaa katika kitongoji cha Dansoman jijini Accra kwa wazazi Nan Poku Kwarteng na Beatrice Oppong Martin. Alikulia mjini Accra.
Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Seven Great Princess iliyopo Dansoman jijini Accra kisha alikwenda high school katika shule ya Wasichana ya Methodist huko Mamfe, Akuapim katika mkoa wa Mashariki nchini humo.
Ebony hakumaliza elimu hiyo akaacha shule na kwenda zake ili aweze kujikita zaidi katika sanaa ya muziki. Single yake ya kwanza aliitoa Desemba mwaka 2015.
Mnamo Machi 2016 alirudi na single kali iliyompa umaarufu ya Kupe na kuanzia hapo nyota yake ilianza kung'ara hadi mauti yalipomkuta.
0 Comments:
Post a Comment