Monday, February 17, 2020

KCMC kupima bure Figo Machi 12

Imeelezwa kuwa magonjwa mbalimbali ikiwamo kisukari, shinikizo la damu na uzito  mkubwa yanachangia kwa kiasi kikubwa maradhi ya figo.

Licha ya maradhi hayo kuwa na gharama kubwa ya matibabu, watu walio wengi hawaoni umuhimu wa kwenda kupima afya zao  mara kwa mara na kutibu magonjwa yanayochangia  uharibifu huo wa figo.

Katika kuiona changamoto hiyo hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) inatarajiwa kuanza kutoa vipimo bure ikiwemo upimaji wa figo kuelekea Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kwa taasisi hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na afisa uhusiano wa hospitali hiyo, Gabriel Chiseo, wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo  alisema huduma hizo zitatolewa kuanzia Machi 12 mwaka huu, na tayari mashine zaidi ya 35 za kusafisha damu zimeandaliwa.

Alisema zipo sababu nyingi zinazochangia kuharibika kwa figo,  na kisukari kinaongoza  kwenye orodha hiyo na mgonjwa anahitaji kuwa makini kutafuta masharti ili kujiepusha na ugonjwa huo.
Chiseo anawashauri watanzania kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka na kuepuka matumizi mabaya ya dawa bila kupata ushauri kutoka kwa daktari ili kuepuka magonjwa hayo kuwapata.

”Machi 12 mwaka huu dunia inaazimisha siku ya figo na siku hiyo watakwimu watakuja hapa KCMC na kuwaelezea namna figo ambayo imekuwa ni changamoto na kwa hapa KCMC tayari kuna mashine tano za kusafisha damu kwa ajili ya watu wenye matatizo ya figo, na tunadhani hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu tutakuwa na zaidi ya mashine 30 ambazo zitakuwa zikisafisha watu wenye matatizo ya figo,”alisema.

Aidha aliongeza kusema kuwa “Wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na viunga vyake tunawahamasisha siku ya Machi mosi hadi siku ya kilele ambayo itakuwa ni Machi sita  ambapo tutaazimisha kilele cha taasisi yetu ya miaka 50 tutakuwa na zoezi la upimaji  bure tutaweka mabanda yetu na wananchi watakaofika watahudumiwa bila malipo na watapata elimu juu ya madhara yanayosababishwa na matatizo ya figo na jinsi inavyoshindwa kufanya kazi,”alisema.

Afisa uhusiano huyo alifafanua kwamba utoaji wa huduma hiyo ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli ambayo inaelekeza kuweka mipango thabiti ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ambayo yalikuwa hayatolewi hapa nchini.

Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2011, asilimia 70 ya watu wanaoishi  kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania, idadi kubwa watakuwa wameathirika na maambukizo ya figo ifikapo mwaka 2023.

Utafiti huo unaibainisha  kuwa Tanzania iko kwenye nafasi ya 54 katika nchi zilizoongoza kwa vifo vinavyotokana na ugonjwa huo na asilimia 1.03 ya wananchi wake hufariki kila mwaka.

STORY BY: Kija Elias, Moshi...........................................................Feb 17, 2020

0 Comments:

Post a Comment