Friday, February 7, 2020

Wakulima wa Ndizi washauriwa kutumia Teknolojia ya Viinitete kupata soko zuri


Wakulima wa ndizi mkoani Kilimanjaro wameshauriwa kutumia mbegu safi za viinitete (Tissue Culture) kwa matokeo bora na uzalishaji wenye tija. 

Akizungumza katika uzinduzi wa maabara ya viinitete ya Maua Mazuri uliofanyika mjini Moshi Februari 6 mwaka huu, Mtafiti Mwandamizi wa Chuo cha Utafiti wa Kilimo-Maruku Dkt. Mpoki Shimwela alisema changamoto kubwa kwa Wakulima wa Zao la Migomba ni magonjwa na wadudu kama Mnyauko (BXW), Mnyauko Fyuzali (Panama) Wadudu Banana Bungua (Banana Weevils).

"Mbegu bora na safi ni suluhisho la hayo yote mkulima atakuwa na uhakika wa kupata mavuno mengi na safi katika kiwango cha Kimataifa," alisema Dkt. Shimwela.

Aidha Dkt. Shimwela aliongeza kuwa mkulima anayetumia viinitete akitunza shamba vizuri atajipatia mavuno makubwa kwa takribani misimu mitatu bila kupata maambukizi ya magonjwa huku akisisitiza changamoto ya masoko.

"Bado tuna changamoto ya masoko, wafanyabiashara wamekuwa wakiwanyonya wakulima wananunua kwa bei ya chini na kwenda kuuza kwa juu," aliongeza Dkt. Shimwela.

Pia Dkt. Shimwela alisisitiza kuwa vyama vya ushirika vitaundwa endapo kutakuwa na vikundi vidogo vidogo vya wakulima wa ndipo. 

"Tupo katika kulifanyia kazi. Tumekuwa tukiwahamasisha waliopo kwenye vikundi hivi na kuvisajili ili vitambulike,Nimeenda Uganda wenzetu wana vyama vya ushirika, tukiuza kwa pamoja itakuwa na maana mkulima mmoja mmoja hataweza." alisema Dkt. Shimwela.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Masuala ya Kilimo kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Fred Massawe alisema miche ya kisasa inatoa ukinzani dhidi ya magonjwa na Mkulima ataongeza uzalishaji wake. 

"Maabara za Viinitete vya Migomba zikiiendelea kufunguliwazitasaidia kupunguza bei za miche hiyo ya kisasa na bei nafuu zaidi katika usambazaji ili mkulima aweze kumudu kununua miche hiyo nijambo la kuzingatia," alisema Massawe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Maua Mazuri Jan Harm Beukema alisema Maabara ya Maua Mazuri ilianzishwa 2018  kwa malengo ya kuzalisha viinitete bila kutumia kemikali yoyote ili kupata mazao bora.

"Miaka mitatu baadaye tutaweza kuzalisha miche milioni tatu hadi tano kwa mwaka, lakini kwa  sasa tunazalisha miche laki tano na Mei mwaka huu tunarajia kupata mazao ya kwanza baada ya kuandaa miche hiyo kwa njia ya viinitete", alisema Beukema.

Tanzania ni nchi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Uganda katika ukulima wa ndizi licha ya kwamba kiasi kikubwa cha uzalishaji huo ni kwa ajili ya chakula. Aidha ndizi ni zao la nne la mazao ya wanga kwa matumizi baada ya Mahindi, mchele na mihogo. 

STORY BY: Jabir Johnson, Moshi...........................................Februari 7, 2020.
Gazeti LaJIJI  2020 likiwa na makala ya Viinitete vya Ndizi 


0 Comments:

Post a Comment