Wenyeviti wa Mabonanza ya Maveterani Kanda ya Kaskazini wamekubaliana kutumia vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kutibu tatizo sugu ambalo limekuwa mwiba katika mashindano mengi ya maveterani katika kanda hiyo.
Makubaliano hayo yalifikiwa hivi karibuni baada ya klabu tatu za maveterani kutoka Arusha na Kilimanjaro kukutana katika mkutano wao wa kufungua mwaka 2020 uliofanyika katika viunga vya Shule ya Sekondari ya Ilboru kujadili namna wanavyoweza kuboresha mabonanza ya klabu hizo.
Klabu ya Kitambi Noma, Arusha All Stars zote za Arusha na Moshi Veterans Club kutoka Kilimanjaro zilikubaliana kutumia utaratibu huo ili kuwabaini wanaoingia kucheza mechi za maveterani wakati umri wao hauruhusu au ushiriki wa wachezaji wanaocheza ligi.
Akichangia mchango wake Makamu Mwenyekiti wa Kitambi Noma John Mhala alisema, "Tunazingatia umri zaidi ya miaka 35 ili tujenge maana ya mashindano ya Maveterani, baadhi ya waandaji wamekuwa wakitoka nje ya maana halisi ya maveterani Rais (Magufuli) ameshaongeza muda hivyo hakutakuwa na kisingizio", alisema Mhala
Kwa wale watakaokuwa wakishiriki kutoka nje ya Tanzania, Mhala aliongeza, "Kwa mfano wa Kenya tumeshawapa taarifa wao watakuja na kitu wanakiita kipande (passport) hiyo itakuwa uthibitisho wetu, tofauti na hapo wasiokidhi watakuwa watazamaji."
Mwenyekiti wa Arusha All Stars Dennis Shemtoi alisema katika mabonanza mengi ya maveterani kumekuwa na wachezaji wasiokuwa na hadhi ya kuzichezea klabu za maveterani kutokana na wengi wao kucheza ligi hivyo uwiano umekuwa ukikosekana na malengo ya undugu na mshikamano kutofikiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti Tumaini Mungete wa Moshi Veterans Club alisema Vitambulisho vya Taifa vimerahisisha kuratibu shughuli mbalimbali ikiwamo michezo kwani udanganyifu umekuwa mkubwa kwa maslahi ya wachache hali ambayo imekuwa ikiwaathiri pakubwa na kwamba watasimamia kwa nguvu zote wakati utakapofika kwa kila mshiriki.
Kitambi Noma imekuwa ikiandaa bonanza lake wakati wa Pasaka maarufu Easter Bonanza, Arusha All Stars imekuwa ikiandaa bonanza kila mwezi wa nane hususani wakati wa Sherehe za NaneNane na Moshi Veterans Club imekuwa ikiandaa bonanza lake mwezi wa 12 maarufu Madesho Bonanza.
STORY BY: Jabir Johnson..........................Arusha; Januari 27, 2020
0 Comments:
Post a Comment