Maelfu ya Wakenya kutoka maeneo mbali mbali wamehudhuria ibada maalum ya kumuaga rais mstaafu Daniel Toroitich arap Moi katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na wakuu na viongozi mbali mbali wakiwemo, viongozi kutoka mataifa jirani kama vile Tanzania, Rwanda, Uganda, na Sudan Kusini.
Moi alifariki siku ya Jumanne wiki iliopita.
Katika hotuba yake rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kwamba anamsherehekea Moi kama kiongozi na mwanahistoria. Alikuwa kiongozi aliyeweza kutabiri hali ya siku zijazo ya kisiasa.
Alisema kwamba uongozi wake wa kutaka kuleta amani ulipita mipaka.
Aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga alisema kwamba ijapokuwa mzee Moi alikuwa na makosa alisaidia katika kutengeneza katiba mpya mbali na kuleta elimu kwa wote pamoja na maziwa ya nyayo. Raila alisema kwamba mzee Moi anafaa kukumbukwa kwa mazuri aliyotenda badala ya mabaya anayohusishwa nayo.
Kwa upande wake makamu wa rais William Ruto alisema kwamba Moi anapaswa kuheshimiwa kwa kuleta makabila yote serikalini.
Aliusema kwamba ijapokuwa hakuwa kamili kama mwanadamu mwengine yoyote yule miaka mitatu iliopita alikuwa akilitakia mema taifa hili.
Rais mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki ambaye hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake alisema kwamba rais Moi aliliongoza taifa la Kenya kama kiongozi thabiti.
Alisema kwamba aliwahudumia Wakenya kwa kipindi kirefu mbali na kukabidhi mamlaka kwa mrithi wake kwa njia ya amani wakati alipostaafu.
0 Comments:
Post a Comment